Balozi wa Indonesia hapa nchini Prof. Dkt. Rahlan Pardede amefanya ziara Mkoani Lindi ambapo ametembelea na kujionea fursa mbalimbali zilizopo kwa ajili ya Wanalindi na Waindonesia. Akiongozwa na mwenyeji wake Mhe. Zainab Telack, Mhe. Balozi alipata nafasi ya kujionea fursa za Lindi kupitia mada zilizowasilishwa na Afisa Mkuu wa Maendeleo ya Jamii Mkoa Ndg. Gaudence Nyamihura pamoja na Dkt. Bora Haule (mwekezaji binafsi) kabla ya Mhe. Balozi kuwasilisha fursa zilizopo nchini Indonesia.
Baada ya mawasilisho yaliyofanyika ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Balozi alifanya ziara ya siku mbili ambapo alhamisi ya tarehe 03 Agosti 2021 alitembelea shamba la chumvi la jeshi la magereza, shamba la minazi lililopo mtaa wa Ng’apa pamoja na Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi, VETA kilichopo mtaa wa Mitwero. Mhe. Balozi alihitimisha ziara yake siku ya Ijumaa ya tarehe 04 Agosti 2021 kwa kutembela na kujionea shughuli za uchimbaji mawe ya gypsum katika kijiji cha Kilanjelanje Wilayani Kilwa na kisha alitembelea hifadhi ya urithi wa utamaduni wa Dunia Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Mhe. Balozi amefurahishwa na shughuli za uzalishaji na huduma alizoziona na kuahidi kutoa mchango wake kwenye maeneo ya utaalam, usindikaji wa bidhaa ghafi, ufungashaji wa bidhaa, vifaa vya mafunzo, masoko ya bidhaa zinazozalishwa Mkoani Lindi. Akiwa kwenye shamba la minazi lililopo mtaa wa Ng’apa Mhe. Balozi amewataka wafugaji wa samaki na wakulima wajisajiri kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wizara ya Mambo ya Nje ili wapatiwe mafunzo ya kitaalam kwenye ufugaji samaki na kilimo kupitia program ambayo ipo tayari.
Mhe. Zainab Telack akionesha kufurahishwa na ujio wa Mhe. Balozi Mkoani Lindi amemshukuru Balozi huyo kwa ahadi zote za kuusaidia Mkoa wa Lindi lakini amemuomba pia ahamasishe wawekezaji wa Indonesia wachangamkie fursa tulizonazo na kuja kuwekeza Lindi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.