Bi. Madenge: Simamieni haki za binadamu.
Watendaji wa kata wilaya ya Lindi wametakiwa kusimamia haki za binadamu na upatikanaji haki kisheria.
Hayo yamesemwa na Bi. Rehema Madenge, Katibu Tawala Mkoa wa Lindi wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa kata kuhusu haki za binadamu na upatikanaji haki kisheria yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi.
Bi. Madenge amesema watendaji wanao wajibu mkubwa wa kusimamia haki na upatikanaji haki kisheria. Hii ni pamoja na usimamizi wa haki za watoto ambapo kwa mkoa wa Lindi kumekuwa na tatizo kubwa la mimba za utotoni kunakopelekea watoto hao kukosa haki zao za msingi.
“Katika mkoa wa Lindi tuna tatizo kubwa la mimba za utotoni hivyo ni lazima mtambue kuwa jambo hili linasababisha watoto kukosa haki zao ikiwa ni pamoja na haki ya elimu. Hivyo ni matarajio yangu kuwa mtakapo toka hapa mtakwenda kupambana na mimba za utotoni kwa kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua stahiki”, alisema Bi. Madenge.
Vilevile kuna makundi mbalimbali ambayo hushindwa kupata haki au kudai haki kisheria hasa ya walemavu kuanzia kwenye ngazi ya familia. Hivyo watendaji wametakiwa kwenda kutoa elimu hii kwenye maeneo wanayotoka ikiwa ni pamoja na matumizi ya madawati ya kijinsia yanayoratibiwa na polisi.
Pia Madenge amewataka watendaji hao kutumia mafunzo hayo kubadilishana uzoefu kwa kuzungumza mambo yanayowakwamisha kiutendaji na kujadili namna ya kuboresha.
Aidha, Bi Madenge amewashukuru Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, chini ya ufadhili wa Legal Service Facility (LSF) kwa kuandaa mafunzo haya ambayo yataleta tija kubwa katika kuboresha utendaji na hatimaye kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi.
Akizungumza kabla ya ufunguzi Alexander S. Hassan, Mkurugenzi Elimu kwa Umma na Mafunzo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ambayo yalifanyika tarehe 7-11 January, 2019 yaliyowahusisha baadhi ya wakuu wa idara wa sekretarieti ya mkoa na halmashauri za mkoa wa Lindi.
Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo watendaji wa kata kuhusu misingi ya utawala bora na haki za binadamu ili waweze kutumia elimu watakayoipata kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Katika mkoa wa Lindi mafunzo haya yatafanyika katika wilaya tatu za Lindi (Lindi DC na Lindi MC), wilaya ya Liwale (Liwale DC na Kilwa DC) na wilaya ya Ruangwa (Ruangwa DC na Nachingwea).
Naye Emmanuel Lweyo, Afisa Utumishi manispaa ya Lindi (Mwezeshaji) amesema mafunzo haya ni muhimu kwa watendaji kwani yapo mambo mengi ambayo yamekuwa yakifanyika kutokana na kutokuwa na uelewa kwa watendaji. Watendaji wanapaswa kuelewa mipaka yao ya kiutendaji kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuweza kutoa huduma kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Issa Mbaruku, Mtendaji wa Kata ya Kitumbikwera (Mshiriki wa mafunzo) ameshukuru kupata mafunzo hayo kwani yamemsaidia sana kuhusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto wa kike. Issa amesema katika jamii hilo tatizo lipo hivyo wananchi wanatakiwa kuelimishwa zaidi juu ya namna ya upataji haki kisheria.
Pia amesema wao kama watendaji watakwenda kusimamia maagizo yaliyotolewa na Katibu Tawala Mkoa hasa katika kusimamia na kudhibiti mimba zo utotoni. Hii ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote watakaohusika na kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa haki za watoto.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.