Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omary amesisitiza kuendelea kutoa elimu zaidi juu ya mpango wa huduma ya usafiri wa dharura ujulikanao kama M-mama.
Bi. Zuwena ameyasema hayo akiwa ni mgeni rasmi katika kikao cha makabidhiano ya mpango wa M-mama kati ya serikali na wadau baada ya kukamilisha kipindi cha ushirikiano wa moja kwa moja kilichofanyika siku ya jumatatu, tarehe 09 Oktoba 2023 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kikiwahusisha viongozi wa Mkoa, Wilaya, tamisemi, Pathfinder na Touch Foundation.
Bi. Zuwena akiwashukuru wadau waliofanikisha mpango huo ambao ni USAID, Vodafone Foundation, Pathfinder na Touch Foundation, amesema kuwa Mkoa unapoenda kutekeleza mpango wa M-mama bila wafadhili ni vyema kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kuielimisha jamii juu ya umuhimu na matumizi sahihi ya utoaji na upatikanaji wa taarifa za wanufaika.
Ameongeza kuwa jamii ielimishwe vizuri kuhusiana na matumizi sahihi ya namba ya simu ya huduma kwa mteja ili isigeuke kuwa kero na usumbufu kwa matumizi ambayo hayatoendana na malengo husika.
" Elimu, uhamasishaji na ushirikishaji wa jamii ikiwemo viongozi wa ngazi zote ili kuhakikisha elimu kuhusu huduma ya usafiri wa dharura inatolewa kwa umma." Amesema Bi. Zuwena.
Pamoja na elimu ya mpango mzuri wa huduma ya M-mama, Bi. Zuwena amewataka wataalam wa afya kuongeza nguvu katika kutoa elimu ya chakula na lishe bora kwa mama mjamzito na mtoto ili isaidie kuondokana na changamoto ya tatizo la udumavu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi Dkt. Kheri Kagya amesema kuwa mpango wa M-mama tangu aunze kutekelezwa Mkoani Lindi mwaka 2022 umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya vifo vya mama na mtoto.
Kutokana na umuhimu na mafanikio makubwa ya mpango wa M-mama, Dkt. Kagya ameongeza kuwa Mkoa wa Lindi umejipanga vizuri kuendelea na utekelezaji wa mpango huo ambao unaenda kutekelezwa kwa asilimia 100 na Serikali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.