Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga Jumla ya bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mifugo mkoani Lindi.
Hayo yemesemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega alipofanya ziara ya siku nne kuanzia tarehe 20-23 Septemba 2021 ya kuwatembelea wakulima na wafugaji kwa lengo la kutatua migogoro kati ya makundi hayo mawili. Mhe. Naibu Waziri ameeleza kuwa jumla ya fedha takribani bilioni 1 zitatumika kabla ya msimu wa mvua kuanza mwaka huu 2021 katika ujenzi wa mabwawa mawili katika vijiji vya Kimambi Wilayani Liwale na Matekwe Wilayani Nachingwea, pamoja na majosho katika wilaya hizo ikiwemo na Wilaya ya Lindi.
Mhe. Naibu Waziri akizungumza na wakulima na wafugaji katika vikao vilivyofanyika vijiji vya Kimambi na Mirui Wilayani Liwale, kijiji cha Kilimarondo Wilayani Nachingwea, kijiji cha Nangulugai Wilayani Ruangwa na mtaa wa Miangala Wilayani Lindi, ameeleza kuwa miundombinu hii itatatua migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo kwa asilimia kubwa inasababishwa na changamoto ya uhaba wa maji. Katika ujenzi wa malambo hayo, Mhe. Naibu Waziri amewataka wakandarasi pamoja na wasimamizi ngazi ya wilaya kuwashirikisha wafugaji ili mabirika ya mabwawa hayo yajengwe kwa kuzingatia mahitaji ya wafugaji hao na ikiwa kutakuwa na maboresho zaidi waombwe wafugaji na Halmashauri kuchangia gharama hizo.
Pia Mhe. Naibu Waziri amezitaka Halmashauri kuanzisha na kuboresha miundombinu ya minada ya mifugo ili kuongeza vyanzo vya mapato. Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika kijiji cha Kilimarondo, Mhe. Naibu Waziri amewataka wafugaji wabadilike na waanze kuuza mifugo yao kwa kutumia minada iliyopo ili kuboresha maisha yao na Halmashauri kupata kipato. “ wafugaji vuneni mifugo kwa kuwauza ili mchangie pato la Halmashauri”, amesema.
Katika kikao cha majumuisho ya ziara ya Mhe. Naibu Waziri kilichofanyika tarehe 23 Septemba 2021 Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, akioneshwa kusikitishwa na migogoro ya wakulima na wafugaji Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainabu R. Telack amemweleza Mhe. Ulega kuwa licha ya mifugo kuwa chanzo cha migogoro lakini hayuko tayari kuvumilia mifugo ambayo haichangii pato lolote ndani ya Mkoa “ Mazao ya ufuta na korosho yanaingiza mabilioni ya fedha kwenye Halmashauri zetu, lakini mifugo haina mchango wowote wa mapato….kwetu sisi haina faida.” Amesema Mhe. Telack.
Katika mikutano yake, Mhe. Naibu Waziri ameendelea kuwasisitiza wafugaji na wakulima kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria za nchi, huku akiwaasa wafugaji kuwa miundombinu ya maji inajengwa na Serikali hivyo waache visingizio vya kuvamia maeneo ambayo hayakutengwa kwa ajili ya shughuli za mifugo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.