Bilioni 10.4 zaboresha miundombinu ya Afya - Lindi.
Mkoa wa Lindi umepokea bilioni 10.4 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na hospitali za wilaya.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM 2015-2020 katika kipindi cha Julai – Desemba, 2019 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Lindi.
Mkuu wa mkoa Zambi amesema katika kuboresha huduma za afya, serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetoa fedha za kujenga na kukarabati vituo vya afya 14, ujenzi wa hospitali za wilaya 2 (Ruangwa & Mtama) na ujenzi wa wodi ya kujifungulia 1(Nachingwea).
Katika awamu ya kwanza mkoa ulipokea Tsh. 1,500,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa vituo 3, awamu ya pili tulipokea Tsh. 5,100,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa vituo 10, na awamu ya tatu mkoa ulipokea Tsh. 3,800,000,000/= ikiwa Tsh. 400,000,000/= fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Nanjirinji, Tsh. 400,000,000/= fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi na watoto katika hospitali ya wilaya ya Nachingwea, Tsh. 1,500,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa hospitali Wilaya - Ruangwa na Tsh. 1,500,000,000/= fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Lindi.
“Ujenzi na ukarabati huu wa vituo vya afya ni kwa ajili ya kuongeza majengo ya maabara, upasuaji, mama na watoto, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya mtumishi. Kwa kufanya hivi serikali imepunguza sana tabu waliyokuwa wanapata wananchi ambao walilazimika kwenda mbali kufuata huduma hizo hasa akina mama wajawazito”, alisema Zambi.
Kwa upande wa zahanati, mkuu wa mkoa Zambi alisema kuna jumla ya zahanati 53 ambazo zinaendelea kujengwa na zipo katika hatua mbalimbali katika halmashauri zote 6 (Manispaa ya Lindi - 5, Halmashauri ya Mtama - 11, Liwale - 3, Kilwa -10, Ruangwa -11 na Nachingwea – 13). Kati ya hizo zahanati 5 zimekamilika zinasubiri kusajiliwa na serikali kuu katika bajeti 2020/2021 ili ziweze kutoa huduma. Zahanati hizo ni Faraja na Chikundi zilizopo halmashauri ya Ruangwa na Kisingo, Miumbu na Mtepera zilizopo halmashauri ya Kilwa.
Aidha, mkuu wa mkoa Zambi amesema serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya afya lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora jirani na maeneo yao.
Katika kuboresha huduma za afya serikali pia imeendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa madawa ambapo kwa mkoa wa Lindi upatikanaji wa dawa katika vituo vyote 253 vya kutolea huduma dawa na vifaa tiba zinapatikana kwa asilimia 93.
Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi, Fadhili ameipongeza serikali kwa kazi kubwa inayofanyika katika kuboresha huduma za afya ambapo mkoa wa Lindi umepatiwa bilioni 10.4 kwa ajili ya kazi hiyo.
Pia ameiomba serikali kuendelea kuboresha huduma za afya katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na kuongeza watumishi ili miundombinu hiyo itakapokamilika wananchi wapate huduma toka kwa wataalam. Aidha, ameishukuru serikali ya mkoa kwa ushirikiano uliopo kati ya chama na serikali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.