Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imezindua rasmi zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa maafisa ugani wa zao la korosho katika halmashauri za mikoa inayozalisha korosho ambapo jumla ya pikipiki 95 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 297 zimetolewa kwa Halmasahuri za mikoa ya Lindi, Mtwara ,Tanga, Pwani, Mbeya, Songwe, Morogoro na Iringa.
Uzinduzi huo umefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, septemba 22, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga, akiambatana pamoja na Mkurugenzi wa bodi ya korosho Francis Alfred, Mwenyekiti wa bodi hiyo Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Daniel Mwanjile.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amesema kuwa
“Kazi tuliyonayo ni kuhakikisha tunapunguza mabonde na tupande ili tuweze kufikia tani 400,000 kama ambavyo mheshimiwa waziri alivyoagiza, Mimi naamini kupatikana kwa vyombo hivi vya usafiri kwa wataalamu wetu unaenda kurahisisha utendaji wao wa kazi na kuhakikisha wanawafikia na kuwapatia ushauri bora wa kilimo kwa wakulima wote wa korosho katika maeneo yao”.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewataka maafisa kilimo kuwatembelea wakulima wa korosho na kuwapa ushauri wa kitaalam ambao utasaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kufanikiwa kufikia lengo la mkoa la kuwa namba moja kwa uzalishaji kitaifa.
“Lengo mkoa wa Lindi ni kuwa kinara wa uzalishaji wa korosho na inawezekana, wataalamu wetu kutoka Naliendele tunapokaa nao wanatutia moyo kwamba sisi tunaweza kwa sababu mazingira yote ambayo yanatuwezesha kuwa namba moja kwa uzalishaji korosho tunayo”.
Mwanzo akizungumzia kuhusu ugawaji wa pikipiki hizo mwenyekiti wa bodi ya korosho, Brig. Jen Mstaafu Aloyce Daniel Mwanjile alisema kuwa,
“Chimbuko la tukio letu hili la leo ni mkutano mkuu wa wadau wa korosho wa mwaka 2021,ambapo pamoja na mambo mengine uliagiza bodi ya korosho Tanzania kusaidia upatikanaji wa vitendea kazi kwa maafisa kilimo wakiwamo waratibu wa zao letu la korosho wa halmashauri ili waweze kuwafikia wakulima vijijini na kuwapatia huduma za ugani, Ninayo furaha kukuambia kuwa pikipiki unazoenda kuzizindua nakuzigawa punde ni utekelezwaji wa agizo hilo.”
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa ccm mkoa wa Lindi ndugu Rajab Siraj amesema Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Lindi kinaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na serikali kuchochea maendeleo ya wananchi wa mkoa wa Lindi.
“Na sisi kama chama tutaunga mkono kutumia vizuri wataalamu wetu ambao leo wanapatiwa vitendea kazi, tuko nao pamoja, tunaipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha kilimo chetu cha korosho na kuwaboreshea wataalamu wetu ili waweze kutoa huduma inayopaswa kwa wakulima wetu, kwa niaba ya mwenyekiti niseme tu kuwa tunathamini hili zoezi, teundelee, tuko pamoja na tutashirikiana kwenye utekelezaji.”
Katika uzinduzi huo jumla ya pikipiki 23 za awali zimegaiwa kwa watendaji wa zao la korosho wa halmashauri za mkoa wa lindi ambapo halmashauri za mtama,nachingwea, liwale, kilwa na ruangwa zimepata pikipiki nne kwa kila halmashauri huku halmashauri ya manispaa ya lindi ikipata pikipiki tatu.
Ikumbukwe kuwa mara ya mwisho kwa watendaji hao kupewa pikipiki ilikuwa mwaka 2013/14 ambapo pikipiki jumla ya 43 zilitolewa kwa halmashauri 43 zinazolima korosho hapa nchini, hivyo ugawaji wa pikipiki kwa wataalam wa kilimo utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na kuadhiri malengo ya uzalishaji wa korosho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.