Chuo Kikuu cha Dar es salaam kupitia timu ya wakufunzi chuo hicho wamewasilisha rasmi mpango wa ujenzi wa Kitivo cha Kilimo Mkaoni Lindi kwenye kikao kilichofanyika leo tarehe 06 septemba 2021 kwenye Ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi. Akiwasilisha mpango huo mbele ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Zainab Telack, Dkt. Mkabwa L. Manoko amesema utekelezaji wa ujenzi huo unatarajiwa kuanza mwezi huu wa Septemba 2021 eneo la Ngongo, Manispaa ya Lindi lenye ukubwa wa hekta 45.5.
Utekelezaji wa mradi huo mkubwa unakusudia kukuza muundo wa shahada ya kwanza, ubora wa programu na utoaji wa huduma unaoendana na kilimo cha mtanzania, hii ikiwa ni lengo lililowekwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuanzisha na kuendeleza tawi la chuo cha kilimo na teknolojia ya chakula Mkoani Lindi mpaka kufikia juni 2025.
Shughuli zilizopangwa kufanyika kwa mwaka wa fedha 2021/22 kuhusiana na ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam-Lindi (CKL) ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya mihadhara (vyumba vya kufundishia), ofisi za wafanyakazi, maabara, bweni la wanafunzi pamoja na ununuzi wa samani, vifaa vya TEHAMA, mtambo wa kuchakata chakula, vifaa vya maabara za mazao ya kilimo , chakula na uhandisi kilimo.
Kwa mujibu wa mpango wa ujenzi huo mpaka kufikia 2027, eneo la hekta 45.5 ni dogo kutosheleza mahitaji ya Kampasi hiyo hivyo Chuo Kikuu kimeomba kipatiwe eneo lenye hekta 500 zaidi lililopo mtaa wa Nandambi ili kuweza kufanikisha huduma za chuo ikiwa pia ni fursa ya kutumia bwawa la Rutamba kwa mahitaji ya mafunzo. Pamoja na maombi hayo ya ardhi, pia Dkt. Mkabwa alieleza kuwa ili kufikia malengo changamoto za miundombinu ya barabara, maji na umeme zinazoukabili mtaa wa Nandambi zifanyiwe kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack akionesha kufurahishwa na ujio wa mradi huo wa kipekee Mkoani Lindi, amezielekeza mamlaka zote (TARURA, TANESCO Kupitia mradi wa REA) zinazohusika na mradi huo kuhakikisha miundombinu yote ambayo sio mizuri inaboreshwa na kuondoa changamoto zote zilizoelezwa. Akipokea maelekezo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amewahakikishia wakufunzi hao kuwa Wilaya ya Lindi na Manispaa yake wapo tayari kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha huduma za maji na umeme zinapatikana eneo husika. “ Mahala ambapo kuna uwekezaji wowote hizi huduma ni wajibu wetu sisi kuzifikisha……barabara, maji, umeme na kila ambacho kinahitajika kitapatikana kwa haraka kadri itakavyowezekana.”
Uwekezaji wa Chuo cha Kilimo kwa Mkoa wa Lindi ni fursa kubwa kwenye uboreshaji na maendeleo ya kilimo hasa kupitia mazao ya korosho, ufuta, mbaazi, nazi na mazao ya chakula kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.