CRDB yatoa msaada wa mbegu mkoani Lindi
Benki ya CRDB yatoa msaada wa mbegu za mahindi kwa wananchi waliokubwa na mafuriko.
Kama inavyofahamika kuwa mkoa wa Lindi ulipata tatizo la mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyeesha na kusababisha kaya takribani 5,545 zenye watu 28,258 kupoteza makazi, chakula, mavazi na hata fedha. Wananchi hao katika moja ya msaada waliokuwa wakihitaji ilikuwa ni kupatiwa mbegu ili waweze kulima mazao mbalimbali ili waweze kulima na kujikimu na maisha yao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Tully Mwambapa ambaye ni meneja mawasiliano amesema kuwa CRDB ilisikia kilio hicho cha wananchi kupitia kwa Mama Salma Kikwete (Mb) ambaye aliwafuata na kuwaeleza hitaji hilo. Benki kwa kuona umuhimu wake ikaona ni vema kuwasaidia wananchi.
“CRDB imetoa kilo elfu nne (tani 4) za mahindi zilizogharimu milioni ishirini (20) kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mafuriko waweze kulima mahindi yatakayowasaidia kwa chakula na hata biashara”, alisema Mwambapa.
Aidha, Mwambapa aliongeza kusema kuwa walijaribu kutafuta mbegu za aina nyingine za mazao lakini upatikanaji wake ukawa mgumu ndio maana wakaamua kuchukua mbegu za mahindi peke yake. Pia alisema kuwa CRDB ilishaanza kutoa msaada mafuriko yalipotokea kupitia tawi lake la Lindi ambapo walitoa magogoro, mashuka, nguo na nguo za kujisitiri za kina mama.
Mkuu wa mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi ameishukuru benki hiyo kwa kuendelea kutoka msaada kwa wananchi walioathirika na mafuriko kwani wamepoteza kila kitu. Msaada huu utawasaidia kuweza kuzalisha mahindi ambayo yatawasaidi kwa upande wa chakula na biashara kwa watakaofanikiwa kuzalisha vizuri.
Pia ameiomba benki kuendelea kutoa misaada mbalimbali pale panapokuwa na uhitaji na kuendelea kutoa mikopo kwa wananchi wa mkoa wa Lindi ambao wanataka kuwekeza au kufanya biashara. Kwani wapo wananchi wanataka kuyafanya hayo lakini wanakwama kwa kukosa mitaji.
Naye Mhe. Mama Salma Kikwete (Mb) amesema baada ya mafuriko kutokea aliwatembelea wananchi waliokubwa na mafuriko na kupata mahitaji yao ya aina mbalimbali likiwemo na hitaji la mbegu. CRDB alipowafuata kwa ajili ya kuwaomba msaada huo walimkubalia na kuahidi kulifanyia kazi.
Hivyo amewashukuru sana kwa kukubali ombi alilolitoa kwa niaba ya wananchi na kuleta mbegu hizo ambazo zitakuwa ni msaada mkubwa. Pia ameupongeza uongozi wa mkoa kwa kazi kubwa waliyoifanya wakati mafuriko yalipotokea na kuwaomba waendelee kuwa na ushirikiano huo hasa katika kuleta maendeleo katika mkoa wa Lindi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.