Katika kuadhimisha siku ya Unawaji mikono duniani inayofanyika kila mwaka ifikapo Oktoba 15, Shirika la Heart to Heart foundation kwa kushirikiana na KOICA wametoa elimu kuhusu umuhimu wa kunawa mikono kwa wananchi wa kijiji cha Nyangamara A, kata ya Nyangamara kilichopo katika Halmashauri ya Mtama, Wilayani Lindi.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Victoria Mwanziva ameeleza kuwa ni muhimu kwa wananchi kuendelea kuzingatia elimu za afya na kanuni za afya zinazotolewa na wataalamu na kusisitiza kuhusu suala la unawaji wa mikono kama njia mojawapo ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
" Leo ni siku ya maadhimisho ya kunawa mikono duniani, hapa tumeonyeshwa ni kwa namna gani tunaweza kunawa mikono yetu na kuhakikisha ipo safi muda wote sambamba na hilo tunakumbushwa kuhusu usafi wa mikono yetu na miili, usafi wa mazingira pamoja na matumizi ya choo bora. Taasisi hizi za Heart to Heart na KOICA zimekuwa zikitusaidia sisi serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajiri ya afya zetu hivyo ni jukumu letu sisi kama wananchi kuchukua tahadhari ili kujikinga na magonjwa ya milipuko kwani yanakingika kwa kuhakikisha tunaboresha mazingira yetu kwa kuyafanya kuwa safi na kutumia vyoo safi na bora" ameeleza Mhe. Mwanziva.
Afisa mradi wa Heart to Heart Bwana Edward Aloyce ameeleza kuwa wametumia siku ya kunawa mikono dunia kutoa rai kwa wanajamii kujenga na kutumia vyoo bora pamoja na kujenga tabia ya kuweka vyombo vya kunawia maji katika makazi yao.
"Sisi Heart to Heart na KOICA tumeamua kuitumia siku hii kuihamasisha jamii kujenga tabia ya kusafisha mikono yao mara baada au kabla ya kufanya shughuli mbalimbali, kujenga na kutumia vyoo bora sambamba na kuweka vinawa mikono. Uhamasishaji huu tunatarajia kwa miaka mitatu tutakua tumeshafikia kata zote za wilaya ya Mtama kwa ajiri ya kutoa rai ya uboreshaji wa vyoo sambamba na kuendelea na miradi ya ujenzi wa visima vya maji ili wanajamii wanufaike na upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yao" Ameeleza.
Hafla ya maadhimisho ya Siku ya Kunawa Mikono Duniani imeenda sambamba na uhamasishaji wanajamii kujitokeza kwa wingi katika uandikishaji wa daftari la mkazi ili waweze kupata nafasi ya kutumia kwa usahihi haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.