Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amewaonya wakulima wanaoshirikiana na baadhi ya watendaji kutoa taarifa za uongo wakati wa zoezi zima la usajiri wa wakulima katika mfumo ili kuweza kujiongezea idadi ya pembejeo pindi zinapoanza kugawiwa.
Mhe. Ndemanga ameyasema hayo katika Mkutano wa Uzinduzi wa Usambazaji na Ugawaji wa Pembejeo za Ruzuku ya Serikali kwa Zao la Korosho Msimu wa 2024-2025 ambao umezinduliwa hapa katika kijiji cha Kiwalala, Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kwa niaba ya Mikoa yote inayojihusisha na Kilimo cha zao la Korosho.
"Tumeambiwa hapa wakati wa zoezi la utambuzi na usajiri wa wakulima, kuna baadhi ya wakulima kwa kushirikiana na makarani tuliowapa jukumu la kukamilisha kazi hiyo wametoa taarifa za uongo ambapo baadhi yao wamesajiri viwanja vya mipira kama sehemu ya mashamba yao ili tu waweze kupata pembejeo nyingi, kwa mfumo huu tunaotumia sasa tunaenda kudhibiti mianya yote ya udanganyifu na hawa tuliowapata tunaenda kuwapeleka mbele ya sheria. Watumishi wa serikali tunao wajibu wa kudhibiti udanganyifu katika usambazaji wa pembejeo hizi"amesema Mhe. Ndemanga.
Aidha, Mhe. Ndemanga ameeleza kuwa ni dhamira ya serikali kuhakikisha kuwa kila mkulima ananufaika na shughuli anayoifanya na katika kuhakikisha utekelezaji wa dhamira hiyo kumefanyika ma boresho katika sekta ya kilimo hususani katika Zao la Korosho ambapo zaidi ya Bilioni 1 zimetolewa ili kuwezesha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.
"Rais angependa mkulima kuona mkulima mmojmmoja anakuwa na uwezo wa kuboresha maisha yake kwa kuweza kuwa na vyanzo mbalimbali vya kipato, inasikitisha sana kuona mkulima anayefanya mauzo ya mamilioni baada ya muda mchache anaishiwa pesa zote wakati hajawekeza hata katika kuboresha makazi yake au kusomesha watoto wake, niwahusie sana tujifunze nidhamu ya fedha, utajiri hauji mara moja jiwekeze kidogokidogo utafikia malengo yako uliojiwekea"
Vilevile, Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa Bodi ya Korosho Tanzania kuamgalia namna ya udhibiti wa vifungashio na makopo yanayotumika kuhifadhia pembejeo hizo ambazo huzagaa mitaani na katika vyanzo vya maji hali inayotishia usalama wa binadamu kutokana na kutafutiwa matumizi mengine mbadala kama kuhifadhia maji ya kunywa kwa watoto wawapo shuleni na kusababisha uchafuzi wa mazingira hususani katika vyanzo vya maji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.