Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, leo Octoba 29, 2024 akimuwakilisha Mhe. Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Lindi amezindua rasmi zoezi la upandikizaji wa vifaranga vya samaki katika mabwawa mawili ya kufugia samaki yaliyopo Kijiji cha Nahanga, Kata ya Mandawa, Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ambapo jumla ya vifaranga 7,000 vimepandikizwa.
Akisoma risala ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Ngoma amepongeza juhudi za Serikali katika kuanzisha mradi wenye thamani ya Tsh. Milioni 128 ambao unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu chini ya Programu chini ya Programu ya Lishe na Ufugaji endelevu ambapo ameeleza kuwa mradi huo ukitumiwa vyema kwa malengo yaliyokusudiwa utakwenda kubadilisha maisha ya wakazi wa kata ya Mandawa kwa kuongeza kipato, kutoa fursa za ajira na kuboresha lishe miongoni mwa wanajamii na kuongeza kuwa mradi huo utakuwa kichocheo muhimu cha maendeleo katika sekta ya uvuvi wilayani Ruangwa.
Aidha, Mhe. Ngoma ametoa wito kwa wanakikundi wanufaika wa mradi huo na wanajamii kwa ujumla kuhakikisha mradi huo unakua endelevu na unakua wenye manufaa kama yalivyo malengo ya serikali ambayo imeendelea kujipambanua kwa kubuni miradi mbalimbali ya kiuchumi ili kuhakikisha inaboresha maisha ya wananchi wake hususan kuongeza wigo wa fursa za kujiajiri kwa vijana na wanawake.
Ili kuhakikisha mradi huo unakua endelevu, Mratibu wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi Tanzania,amewasisitiza wanakikundi kuhakikisha wanazingatia elimu ya ufugaji wa samaki waliyoipata kupitia mafunzo hususan utengenezaji wa chakula cha samaki na namna ya kuwalisha pamoja na ulinzi wa mabwawa dhidi ya wanyama waharibifu kama Kenge na ndege walao samaki.
Akimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Bwana. Nathalis Linuma amewataka wananchi kuutunza mradi na kuhakikisha moja ya faida yake kubwa ni kuimarisha lishe za wakazi wa kata ya mandawa pamoja na kujiongezea kipato, na kuwasisitiza kushiriki katika zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Mzee Mwigambe, Mkazi wa Kijiji cha Nahanga ameishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo wenye manufaa kiuchumi na kijamii na kuwaomba wananchi wenzake kushirikiana na kuunga mkono juhudi za serikali bila ya kubagua itikadi za vyama vya siasa bali kuangalia mwenendo wa maendeleo yanayopatikana katika maeneo yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.