DKT. BORA ABAINISHA SABABU ZA AKINAMAMA KUTOKUJITOKEZA KUPATA MATIBABU YA FISTULA.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Dkt. Bora Haule amebainisha sababu zinazosababisha akinamama ambao wamepata ugonjwa wa fistula kutokujitokeza kupata matibabu ya fistula katika uzinduzi wa kampeni ya matibabu ya fistula uliofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Lindi.
Dkt. Bora ametoa sababu hizo wakati akizindua mradi huo uliofadhiliwa na kampuni ya Equinor Tanzania ambao umelenga kutoa huduma za matibabu ya ugonjwa wa fistula bure kwa akinamama waathirika mkoani Lindi.
“Fistula ni ugonjwa unaomuondolea mwanamke staha na utu wake kwa kumsababishia kushindwa kuzuia haja ndogo na kubwa ambazo zote hutoka kwa kupitia njia ya uke”, alisema Dkt. Bora.
“Sababu zinazopelekea wanawake wengi kupata fistula ni pamoja na kuchelewa kupata huduma za afya wakati wa ujauzito hasa wakati wanapokaribia kujifungua,kupata mimba katika umri mdogo yaani mimba za utotoni na kukeketwa”, aliongeza Dkt. Bora.
Aidha, Dkt. Bora ameelezea sababu zinazopelekea wanawake wengi kushindwa kujitokeza wanapopata ugonjwa ambazo ni aibu, dhana potofu iliyopo ndani ya jamii ambayo imekua ikiamini kuwa mwanamke anaepata fistula ni yule ambaye ametembea na wanaume wengi wakati wa ujauzito. Pamoja na kushindwa kumudu gharama za matibabu ya fistula yanayojumuisha chakula, usafiri pamoja na gharama za matibabu yenyewe.
Pia amemshukuru mkurugenzi mkazi wa Equinor Tanzania Dkt. Mette Ottoey kwa kuchagua mkoa wa Lindi na kufadhili mradi wa matibabu hayo na kuongeza kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa Lindi itahakikisha hospitali ya rufaa ya mkoa wa Lindi Sokoine inashirikiana na madktari kutoka hospitali ya CCBRT katika kufanikisha zoezi hilo la utoaji wa huduma ya matibabu ya fistula bure kwa wanawake wa mkoa wa Lindi.
Naye mkurugenzi mkazi wa Equinor Tanzania Dkt. Mette amesema anaamini kuwa jitihada wanazozifanya zitasaidia kuimarisha maisha ya wagonjwa walioathirika na ugonjwa wa fistula na zitawawezesha kuweza kurejea kwenye utekelezaji wa majukumu ya kila siku katika kujiletea maendeleo.
Mkurugenzi wa CCBRT, Brenda Msangi amesema wao wamejipanga kuhakikisha wataalam husika wanakuwepo katika kutoa huduma na kwamba wataendelea kuwajengea uwezo wataalam wa hospitali ili hata watakapoondoka huduma ya upasuaji dhidi ya fistula iendelee kutolewa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.