Katika ziara maalum ya Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Seleman Jafo (Mb) wilayani Liwale ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa zahanati mpya katika kijiji cha Ngorongopa hatua ambayo inatarajiwa kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa kijiji hicho na maeneo jirani punde itakapokamilika ifikapo Novemba 30,2024.
Hatua hiyo imekuwa faraja kubwa kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitembea umbali wa kilomita 10 kwenda kijiji jirani cha Nangirikiti hivyo ujenzi wa zahanati hiyo unakwenda kuleta afueni ya changamoto haswa za usafiri kwa wakazi hao hususan akina mama wajawazito, watoto wachanga na wazee.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa zahanati hiyo iliyogharimu Tsh Milioni 50 kutoka serikali kuu, Bwana. Mbaraka Juguju, mtendaji wa kata ya Ngorongopa ameeleza kuwa ujenzi wa zahanati hiyo unakwenda kuwa tiba ya changamoto za huduma ya afya zilizokuwa zinawakabili wakazi wapatao 1219 huku ikisogeza karibu huduma za kujifungua na kliniki kwa wajawazito na watoto.
Dkt. Jafo amewahakikishia wananchi hao kuwa zahanati hiyo itaanza kutoa huduma mara tu ujenzi wake utakapokamilika.
"Niwahakikishie kuwa tayari serikali imeshatoa fedha kwa ajiri ya kununulia vifaa tiba na imeshaelekeza wahudumu wa afya watakaokuja kutoa huduma hapa, hivyo zahanati hii itaanza kufanya kazi mara tu ujenzi wake utakapokamilika Novemba 30 mwaka huu" ameeleza.
Bi. Hawa Abdallah, mama mwenye mtoto mchanga wa siku 9 alikuwepo kushuhudia tukio hilo na kueleza kuwa kabla ya uwepo wa zahanati hiyo wajawazito walikuwa wanachelewa kuanza mahudhurio ya kliniki pamoja na watoto wachanga kutokukamilisha ratiba ya chanjo mbalimbali kutokana na kukwepa gharama za usafiri kwenda Nangirikiti.
"Nina imani kubwa kuwa baada ya zahanati hii kufunguliwa, hatutakuwa na haja ya kutembea umbali mrefu. Wajawazito wataanza kuhudhuria kliniki kwa wakati na hatutolazimika kuwakatiza watoto wetu kupata chanjo zote zinazostahili kama inavyotakiwa. Tunaishukuru sana serikali ya Mama Samia na tunamuombea kwa Mungu ampe afya njema ili azidi kutuhudumia wananchi wake." ameeleza Bi. Hawa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.