Shirika la kimataifa la Girls Effect linaloendesha shughuli zake kwa lengo kuu la kuwafikia vijana na taarifa sahihi kuhusu afya zao siku ya Jumatano wiki hii, tarehe 19 Julai 2023 limezindua rasmi mradi wa uhamasishaji wa chanjo kwa watoto na wasichana Mkoani Lindi ujulikanao kama " Mwanzo Mwema".
Uzinduzi huo umefanyika Wilayani Nachingwea kwenye kikao Maalum kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu, TTC kikiwahusisha Viongozi wa Mkoa, Wilaya, Halmashauri, Viongozi wa dini pamoja na wadau wengine katika sekta ya elimu na afya.
Mradi huo unaofadhiliwa na GAVI the Vaccine Alliance utatekelezwa na Shirika la Girls Effect kwa muda wa miaka minne ambapo umeanza mwaka 2022 mpaka mwaka 2026 na utatoa huduma kwa watoto walio chini ya miaka miwili na wasichana wenye umri wa miaka 14 watanufaika katika Halmashauri za Liwale, Ruangwa, Kilwa na Nachingwea zilizopo Mkoani Lindi.
Kwa watoto walio chini ya miaka miwili, mradi utajikita kuhamasisha jamii kushiriki katika kuwapatia watoto hao chanjo zote muhimu. Pia mradi huo utahamasisha wasichana wa miaka 14 kupatiwa chanjo ya kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi, HPV pamoja na kuboresha tabia za ufuatiliaji wa mambo ya kiafya kwa jamii.
Utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa ushirikiano na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais-Tamisemi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Katavi na Shinyanga.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe.Zainab Telack amelishukuru Shirika la Girls Effect kwa kuamua kuleta huduma zao Mkoani Lindi huku akiomba kuongeza wigo huduma hizo ikiwemo kwenye eneo la kuboresha masuala ya lishe.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi ni vyema Wakuu wa Wilaya husika wakashirikishwa vyema ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.