Wananchi wawakaribisha wawekezaji wa kilimo cha zao la muhogo.
Wananchi wa vijiji vya Mavuji na Migeregere wilayani Kilwa wameikaribisha kampuni ya Pan Tanzania Agriculture Development Limited kuwekeza katika kilimo cha zao la muhogo.
Wananchi hao licha ya kuwakaribisha na kuwapatia wawekezaji ardhi yenye ukubwa wa ekari elfu moja kwa ajili ya kilimo hicho cha muhogo, wameiomba serikali kuhakikisha inaisimamia kampuni hiyo ili itoe ajira nyingi kwa wananchi wa maeneo hayo ili uwekezaji huo uwe na tija kwao. Pia wameomba ufuatiliaji wa mara kwa mara wa matumizi ya ardhi hiyo ufanyike kwani kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wawekezaji kutotumia ardhi kwa malengo yaliyokusudiwa au kukaa nayo bila kuitumia.
Mkuu wa mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi baada ya kushuhudia makubaliano yaliyofikiwa kati ya wananchi na kampuni ya Pan Tanzania Agriculture Development Ltd, aliwahakikishia wananchi kuwa wawekezaji hao wamefuata taratibu zote za kisheria zinazotakiwa kufuatwa na serikali imewaruhusu kufanya uwekezaji wa zao hilo hapa nchini.
Zambi alisema kuwa kampuni hii tayari imeshaanzisha kilimo cha muhogo katika maeneo ya Handeni mkoani Tanga, hivyo lengo lake la kufika hapo ni kama wananchi wamekubali kuupokea uwekezaji huo katika maeneo yao ili serikali ya mkoa ikamilishe taratibu za kuwapatia ardhi uzalishaji uanze.
Aidha, mkuu wa mkoa amewatoa hofu wananchi hao kuhusu lugha ambazo zitatumika katika kuandaa mkataba wa uwekezaji ambapo zitatumika lugha tatu ambazo ni kichina, kiingereza na kiswahili ili kutoa fursa kwa watu wote ambao wanahusika katika makubaliano hayo ya uwekezaji kuelewa kile kilichoandikwa kwa urahisi na ufasaha.
Naye mwekezaji kutoka katika kampuni hiyo, Madam Feng Yingdai amewashukuru wananchi wa vijiji hivyo viwili kwa kuridhia na kuikaribisha kampuni yake ili iweze kufanya uwekezaji katika maeneo hayo. Pia ameahidi kutumia ardhi hiyo kuzalisha zao la mhogo ambayo itauzwa katika soko la dunia. Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa kampuni yake itatoa ajira kwa wananchi wengi wa maeneo hayo na nafasi chache za kitaalamu zaidi zitatolewa kwa watu wenye utaalamu huo.
Katika uwekezaji huo, wakulima binafsi watapata fursa ya kuuza mihogo yao (ambayo imekaushwa maarufu kama makopa) kwa kampuni kwani kampuni ina lengo la kuuza zaidi ya tani milioni mbili za mihogo mikavu kila mwaka. Pia amewatoa hofu wakulima kuwa mbegu watakayotumia ni aina ya kiroba kwani ndio mbegu iliyobora inayopendekezwa na wizara ya kilimo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.