Hakikisheni watoto wanapata chanjo – DC Ndemanga
Mkuu wa wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga amewataka watendaji kuhakikisha kila mtoto chini ya miaka mitano anapata chanjo ya Surua-Rubela na Polio.
Mhe. Ndemanga ameyasema hayo katika kikao cha PHC cha ngazi ya wilaya na halmashauri ya manispaa ya Lindi kilichohusu kampeni ya kitaifa ya utoaji chanjo hiyo kwani kumekuwepo na tatizo la baadhi ya watu kutopeleka watoto kutopata chanjo kwasababu zao binafsi kunakosababisha magonjwa ya mlipuko kuendelea kujitokeza.
Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa sana za kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na utoaji wa chanjo kama hizi bure. Lengo ni kuzuia milipuko zaidi ya magonjwa hayo yanayoweza kujitokeza baada ya watu kushindwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika kupata chanjo.
“Niwaagize wataalam na watendaji wote mnaohusika na zoezi hili la utoaji chanjo kuhakikisha jamii inahamasishwa kujitokeza lakini pili asiwepo mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano atakayekosa chanjo hii kwani suala hili sio la hiari na endapo atajitokeza mtu yeyote atakayebisha hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwa kuwa huyo atakuwa nanataka magonjwa yaendelee kujitokeza katika jamii yetu,” alisema Mhe. Ndemanga.
Aidha, Mhe. Ndemanga amewataka wataalam kuhakikisha katika zoezi la uhamasishaji jamii wahakikishe wanatoa elimu ya kutosha kwa jamii kuhusu umuhimu wa watoto kupata chanjo hiyo na madhara ya kutopata chanjo hiyo ili ieleweke vizuri. Lakini pia ameitaka jamii ya wanalindi kutambua kuwa zoezi hili litakuwa likisimamiwa pia na vyombo vya usalama lengo ni kuhakikisha linafanyika kikamilifu na kufikiwa malengo yaliyowekwa.
Naye mganga mkuu wa manispaa ya Lindi, Dkt. Dismass Masuluhu amesema chanjo hiyo itatolewa kwa watoto zaidi ya elfu 26 katika wilaya ya Lindi ambapo kutakuwa na siku tano za utoaji chanjo. Katika siku nne za mwanzo tutakuwa na maeneo maalum ya utoaji wa chanjo ambapo watu watatakiwa kufika katika vituo vyetu ili kupata chanjo na siku ya tano timu za Afya zitapita katika maeneo mbalimbali ya wananchi.
Dkt. Masuluhu amewaomba viongozi, wataalam mbalimbali na wadau waafya kushiriki katika kuhamasisha na kutoa elimu katika maeneo wanayotoka ili baadhi ya wananchi waache kuwa na imani potofu kuhusu chanjo hizo ambazo zinaatolewa na serikali kwa ajili ya kuwasaidia.
Mstahiki Meya wa manispaa ya Lindi, Mhe. Mohamedi Lidume amesema kuwa uhamasishaji mkubwa na utoaji wa elimu kwa jamii kutasaidia kuondoa uoga na imani potofu zilizojengeka ndani ya jamii.
Zoezi la utoaji chanjo ya Surua-Rubela na Polio kwa watoto chini ya miaka mitano katika manispaa ya Lindi linatarajiwa kuanza rasmi tarehe 15/10/2019 na kufika tamati tareha 19/10/2019.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.