Hali ya maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya UKIMWI mkoani Lindi imeonekana kuwa juu kutokana na uwiano wa takwimu za waathirika na idadi ya wakazi wa mkoa huu.
Akizungumzia kuhusu hali ya maambukizi kwa mkoa wa Lindi katika kikao cha maandalizi ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo kitaifa itafanyika mkoani Lindi mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka huu, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.Kheri Kagya amesema idadi ya waathirika wa ugonjwa huo ni kubwa kuliko asilimia iliyopo kimkoa.
“kwa takwimu za tafiti iliyofanyika mwaka 2016/17 ilibaini nchi yetu ina maambukizi ya asilimia 4.7%, mkoa wetu wa Lindi ulionekana kuwa na maambukizi ya asilimia 0.3% lakini katika mkoa huu tunao watu takribani 25,600 ambao ni wagonjwa wa Ukimwi na wanatumia dawa.”
“kwa hiyo mbali ya kuwa kiwango cha maambukizi kipo chini, lakini ukitafuta namba utakuta tunalo janga la Ukimwi katika Mkoa wetu”
Aidha Dkt. Kagya alitanabaisha kuwa hali hiyo imegusa pia rika ya watoto ambapo Dkt Kagya alisema kuwa, “….kati ya hao wapo zaidi ya 1,200 ambao ni watoto..”.
Dkt. Kagya ameelezea kuwa mkoa utatumia fursa iliyoipata ya kuwa mwenyeji wa maaadhimisho hayo kitaifa kueneza na kupeleka elimu kuhusu janga la Ukimwi kwa wananchi wa mkoa huo na watanzania kwa ujumla.
“Tumepata fursa hii ambayo itatusaidia kupeleka elimu zaidi ya Ukimwi kwa jamii yetu ili watu wetu waendelee kujikinga”.
Katika hatua nyingine Dkt. Kagya amesema wanatarajia kuendesha tafiti nyingine ambayo itatoa takwimu mpya za hali ya maambukizi kitaifa na kimkoa.
“Mwaka huu tutarajie kuna tafiti nyingine itafanyika ambayo itatupa tena hali halisi ya picha ya Ukimwi”
Kuelekea maadhimisho ya siku ya UKIMWI nchini, Dkt Kheri Kagya ameziomba taasisi nyingine ambazo zinajihusisha na utoaji wa huduma za afya kushiriki kwa pamoja katika kufanikisha zoezi hilo ambalo litasaidia kukumbusha uwepo wa janga hilo hapa nchini, na pia kutafakari na kuhamasishana kuhusu namna ya kujikinga, kujilinda na kujiepusha na ugonjwa huo na pia kuwapa usaidizi wa matibabu waathirika wa ugonjwa huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.