Halmshauri zatakiwa kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2018 wanakwenda shule.
Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Ndg. Ramadhani Kaswa ameuagiza uongozi wa wilaya na halmashauri za Mkoa wa Lindi kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanakwenda shule.
Kaswa aliyasema hayo wakati wa kutangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2017 na uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza Januari, 2018 leo katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Kikao hicho kilihudhuria na Kamanda wa Polisi Mkoa, Afisa Usalama Mkoa, Makatibu Tawala Wilaya, Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Elimu wa Wilaya na Wakuu wa Shule.
“Kumekuwepo na tatizo la baadhi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kutofika shule bila sababu zozote za msingi, hivyo naawaagiza viongozi wote katika wilaya na halmashauri kuhakikisha wanafunzi hawa waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2018 mnawafuatilia kuhakikisha wote wanakwenda shule”, alisema Kaswa.
Pia Kaswa amewaagiza wakuu wa shule kuhakikisha wanatoa taarifa mapema kwenye ngazi ya Kata na Wilaya pale ambapo wanabaini kuwa kuna baadhi ya wanafunzi waliopangwa katika shule zao hawajaripoti. Vilevile uongozi wa wilaya umetakiwa kuwachukulia hatua kali wazazi au walezi wote ambao hawataki kuwapeleka watoto wao shule.
Mkoa wa Lindi katika matokeo ya mwaka 2017 umeshika nafasi 14 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara ambapo umefaulisha watahiniwa 11,898 (wav. 5,772 na was. 6,126) kati ya watahiniwa 17,413 (Wav 8,066 na Was 9,347) waliofanikiwa kufanya mtihani. Kwa mwaka 2016 mkoa ulishika nafasi ya 19 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Aidha, Kaswa amewapongeza viongozi wote kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kusimamia mitihani hadi kuchagua wanafunzi. Amewataka viongozi katika ngazi zote kuhakikisha wanaweka mikakati yenye kulenga kuongeza idadi ya watahiniwa wanaofaulu, kuongeza madaraja ya ufaulu na kupunguza kama si kuondoa kabisa mdondoko wa wanafunzi.
Vilevile amewashukuru wadau wa maendeleo ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kusaidia kunyanyua elimu ya msingi katika mkoa wakiwemo EQUIP – T ambao wanafanya kazi nzuri katika kuboresha elimu ya msingi. Pia amewapongeza wananchi ambao kwa sasa wameanza kuonyesha muamko mkubwa katika kufuatilia maendeleo ya elimu ya watoto wao na kupelekea kujitoa katika kuboresha miundombinu katika shule.
Afisa Elimu Mkoa, Bi. Wengi Mchuchuri alitaja baadhi ya changamoto zilizopo zikiwemo ufaulu mdogo katika baadhi ya maeneo kunakopelekea sekondari za maeneo husika kutojaza mikondo, upungufu wa miundombinu (madarasa) kutokana na kuongezeka kwa wanafunzi waliofaulu na Mdondoko Mkubwa kwa wanafunzi wanaoandikishwa Darasa la Kwanza ukilinganisha na wanaomaliza Darasa la Saba kila mwaka.
Aidha, alielezea mikakati iliyowekwa ikiwa ni pamoja na mkoa kwa kushirikiana na halmashauri kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa ufundishaji na ufunzaji ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule ya msingi, kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018, na mkoa kwa kushirikiana na uongozi wa ngazi ya wilaya, tarafa, kata, mtaa, kijiji, jamii na wazazi/walezi kuhakikisha wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza wanamaliza shule.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.