Halmashauri zatakiwa kutenga fedha za upasuaji wa mabusha.
Halmashauri nchini zatakiwa kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuwezesha zoezi la kuwafanyia watu upasuaji wa mabusha.
Hayo yalisemwa na Dkt. Leonard Subi, Mkurugenzi wa huduma za Kinga wakati akiwasilisha hotuba ya Dkt. Faustine Ndugulile (Mb), Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwenye uzinduzi wa huduma za kliniki tembezi kambi ya upasuaji wa ugonjwa wa Mabusha mkoa wa Lindi na Pwani uliofanyika wilayani Nachingwea.
Dkt. Subi amesema halmashauri katika bajeti zake zinapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kuratibu zoezi hilo badala ya kutegemea uratibu wa wizara peke yake. Matumizi ya kliniki tembezi yanasaidia sana kupunguza gharama na kuwezesha wananchi wengi kupata huduma ya upasuaji bure.
“Gharama ya kumhudumia mgonjwa mmoja kwa upasuaji inakadiriwa kuwa ni sh. 272,000, kiasi ambacho ni vigumu kwa mwananchi wa hali ya chini kumudu. Hivyo kwa halmashauri kutenga fedha kutawezesha wananchi kupata huduma hii bure au kwa kuchangia gharama kidogo”, alisema Dkt. Subi.
Aidha, Dkt. Subi amewasihi wananchi wenye tatizo la mabusha katika mkoa wa Lindi kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya upasuaji ambayo inatolewa bure chini ya uratibu wa wizara ya afya na wadau ambao ni The ENDFUND.
Pia ameishukuru timu ya madaktari bingwa wa upasuaji na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNC) inayoongozwa na Dkt. Alexander Mwelange na Madaktari na watoa huduma kutoka hospitali ya wilaya ya Nachingwea kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwafanyia upasuaji wagonjwa wa mabusha ambapo mpaka sasa wagonjwa wote wapo salama na wamerejea kwenye majukumu yao ya kila siku.
Dkt. Subi amewasihi wataalam wa afya na viongozi kwa ujumla kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa huu wa mabusha. Hii imetokana na baadhi ya wananchi kutokuwa na uelewa sahihi wa nini chanzo, dalili zake, na namna ya kujikinga. Pia amewaagiza madaktari bingwa kuendelea kuwajengea uwezo wataalam wa afya katika hospitali zote wanazopita kufanya upasuaji.
Vilevile alieleza kuwa magonjwa ya matende na mabusha yanazuilika hivyo wananchi wanatakiwa kuzingatia maelekezo wanayopewa na wataalam wa afya ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika umezaji dawa kinga tiba ambazo zinatolewa bure na wizara kwa kushirikiana na mikoa na halmashauri.
Akitoa salam za mkoa kwa niaba ya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango ameishukuru serikali kupitia wizara ya afya na wadau wa maendeleo kwa kuratibu zoezi hilo ambalo limekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi wa hali ya chini. Pia alisema kuwa viongozi katika mkoa wa Lindi wanaendelea kuihamasisha jamii kwa wale wenye mabusha kujitokeza ili waweze kufanyiwa upasuaji bila malipo yoyote.
Naye mratibu wa mpango wa taifa wa kuthibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele toka Wizara ya Afya, Oscar Kaitaba amesema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika mikakati ya kupunguza tatizo la magonjwa haya, lengo likiwa ni kuyatokomeza kabisa.
Aidha, aliyataja magonjwa matano yaliyopo katika mpango kuwa ni Trakoma, Usubi, Kichocho, Minyoo ya tumbo, Matende na Mabusha. Wizara katika mikakati yake ya kudhibiti ugonjwa huu inaendelea na utoaji wa dawa za kinga tiba na utoaji wa huduma za upasuaji wa mabusha ili kuboresha afya za wananchi.
Dkt. Mwelange, kiongozi wa timu ya madaktari bingwa amewahakikishia wananchi kuwa huduma hiyo ya upasuaji ni salama hivyo kila aliye na tatizo baada ya kufanyiwa upasuaji atarejea kutekeleza majukumu yake ya kila siku bila tatizo lolote.
Michael Stambuli mkazi wa Nachingwea ameshuhudia kuwa yeye alikuwa na busha na alikwenda kufanyiwa upasuaji ambapo kwa sasa yupo vizuri na anaendelea na shughuli zake za kila siku. Pia baada ya kufanyiwa upasuaji ameshawapeleka wagonjwa watano toka eneo analoishi ambao nao wamefanyiwa upasuaji na wapo salama.
Kliniki hii kwa mkoa wa Lindi itafanyika katika halmashauri za Kilwa, Nachingwea, Ruangwa na halmashauri ya Kisarawe mkoani Pwani na inatarajia kufanya upasuaji wa mabusha kwa watu 800.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.