Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa leo amehitimisha ziara yake ya kukagua miradi ya serikali Mkoani Lindi ambapo ametembelea na kushiriki katika ujenzi wa kituo cha afya kata ya Mvuleni iliyopo tarafa ya Mchinga, Manispaa ya Lindi.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Lindi ameeleza kuwa mradi wa kituo cha afya umeanza kwa hatua ya awali kujenga jengo la wagonjwa, maabara, miundombinu ya kuchomea taka pamoja na shimo la kutupia mifuko ya uzazi. Miundombinu yote kwa hatua ya awali itagharimu jumla ya Tsh. milioni 250 iliyotolewa na serikali.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Mvuleni, Mhe. Majaliwa amempongeza mbunge wa jimbo la Mchinga Mhe. Salma Kikwete kwa kuwasemea wananchi wa jimbo lake vizuri.
Aidha, Mhe. Majaliwa amewaeleza wananchi hao kuwa baada ya kituo hicho cha afya kukamilika, serikali italeta fedha zingine milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mengine ya upasuaji mkubwa na mdogo, jengo la mama na watoto, nyumba ya daktari na chumba cha maiti. Mhe. Majaliwa amesema baada ya kumalizika majengo yote serikali italeta tena jumla ya Tsh. Milioni 250 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kituo hicho, hivyo kufanya jumla yaTsh. Milioni 750 kukamilisha kituo hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack akiahidi kusimamia ujenzi wa kituo hicho, amewapongeza wananchi wa kata ya Mvuleni kwa kutoa ardhi yao kwa ajili ya maendeleo bila malipo yoyote
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.