Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Uwekezaji imeielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza Kasi ya ujenzi wa mradi wa bandari ya Uvuvi inayojengwa Wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi.
Kamati hiyo ya Bunge ikiongozwa na Menyekiti Mhe. David Kihenzile , Mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini imetoa maelekezo hayo alhamisi ya wiki hii baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo mkubwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ukaguzi wa mradi, Mhe. Kihenzile amesema kuwa Serikali imetoa fedha jumla ya Bilioni 282 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Uvuvi ili kuongeza Kasi ya uvunaji wa mazao ya bahari na kusaidia ukuaji wa uchumi. Ameongeza kuwa Serikali imeamua kufanya kazi Sekta zilizoajili watu wengi zaidi ikiwemo kilimo, mifugo na Uvuvi. Hivyo ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza Kasi ya ujenzi wa mradi ili wananchi wanufaike na utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesisitiza kuwa Wizara itazingatia maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Bunge bila kuadhiri Sera, Sheria, Kanuni na taratibu za Serikali.
Mhe. Ulega amesisitiza pia kwa kazi zisizohitaji utaalam mkubwa, vijana wa Wilaya ya Kilwa wapewe nafasi ili ya kuzifanya ili kuongeza uchumi wao na maeneo yanayozunguka mradi.
Mradi wa Bandari ya Uvuvi inayojengwa Wilayani Kilwa itagharimu kiasi cha Sh. Bilioni 282 ambapo mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 7.5.
Bandari hii itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuingiza meli 3 hadi 10 kwa wakati mmoja kulingana na ukubwa wa meli. Pia itakuwa na uwezo wa kuhudumia boti za wavuvi 300 kwa wakati.
Mradi huu unaotekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Kampuni ya Kichina M/s China Harbour Engineering Company Ltd unatarajiwa kukamilika tarehe 24 Septemba 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.