Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali imeoneshwa kutoridhishwa na Usimamizi na uendeshaji wa Mfuko wa Mikopo ya Akina mama, Vijana na Watu Wenye Ulemavu inayotolewa na Halmashauri.
Hayo yamesemwa jana ijumaa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Halima Mdee(Mbunge) kupitia hotuba yake ya ukaguzi katika kuhitimisha ziara ya ukaguzi wa Miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika katika Wilaya za Nachingwea na Lindi.
Akisoma hotuba hiyo mbele ya wajumbe waliohudhuria kikao cha majumuisho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Mdee ameeleza kuwa Halmashauri zina udhaifu katika Usimamizi na Uendeshaji wa Mfuko wa Mikopo ya Akina Mama, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Mhe. Mdee ameainisha kuwa udhaifu mkubwa upo kwenye urejeshaji wa Mikopo inayotolewa kwa makundi hayo matatu ambapo Kwa mwaka 2016/17 hadi 2020/21 Halmashauri ya Wilaya ya Mtama ilitoa kiasi cha TSH. 271.1 milioni na kufanikisha kurejesha Tsh. 121.7 milioni. Manispaa ya Lindi Kwa mwaka 2015/16 hadi 2020/21 ilitoa Mikopo kiasi cha TSH. 228.7 milioni na kufanikisha kurejesha kiasi cha TSH. 99.5 milioni. Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kwenye eneo la Mikopo, Mwenyekiti wa Kamati amesema kuwa Halmashauri ilikikopesha kikundi cha Akina mama kiitwacho Mshikamano kiasi cha TSH. 18 mil lakini kikundi hicho kimerejesha Tsh. 550,000 Tu.
Mhe. Mdee ameendelea kusema kuwa Mikopo hii ya Akina mama, Vijana na Watu wenye Ulemavu inatolewa bila kuzingatia uwiano wa asilimia 40:40:20.
Mhe. Mdee ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kufanya tathmini upya juu ya utaratibu wa kisheria na muundo wa kitaasisi utakaowezesha Usimamizi na uendeshaji bora wa Mfuko huu ili uweze kuleta tija kwa makundi yaliyokusudiwa na kuweza kujikwamua na wimbi la umaskini.
Maeneo mengine yalioanishwa kuwa na changamoto ni pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani, kutokuzingatia miongozo ya Serikali katika matumizi ya mapato ya ndani, uchangiaji mdogo wa mapato ya ndani kwenye Miradi, uchache wa watumishi, pamoja na Usimamizi wa Miradi ya Serikali.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kuwa kutokana na changamoto za urejeshwaji wa Mikopo TAMISEMI imeunda mfumo ambao utavisajiri vikundi na kutoa Mikopo Kwa mfumo huo. Mchakato unaendelea na TAMISEMI imeunda timu ambayo anafanya kazi kuona mfumo mzuri ambao utatumika.
Mhe. Deogratius Ndejembi ameongeza kuwa changamoto ya uchache wa watumishi, Serikali inalifanyia kazi na tayari Serikali imetoa kibali cha ajira za Wahandisi 260.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi ameipongeza Kamati hiyo kwa kazi nzuri waliofanya Mkoani Lindi na kuahidi kushughulikia changamoto zote zilizoelezwa na Kamati.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa imehitimisha ziara ya ukaguzi wa Miradi ya Serikali Mkoani Lindi ambapo imefanya kazi hii kwa muda wa siku tatu tangu tarehe 21 Machi 2023.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.