Kaswa afungua mafunzo ya kutengeneza Mpango wa motisha kwa ajili ya kuwavutia na kuwabakiza watumishi katika vituo vyao vya kazi.
Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Ndg. Ramadhani Kaswa amefungua warsha yenye lengo la kutengeneza mpango wa motisha kwa ajili ya kuwavutia na kuwabakiza watumishi katika vituo vyao vya kazi yanayofanyika katika Hotel ya M.M iliyopo Manispaa ya Lindi.
Warsha hii inayofanyika kwa siku sita imeandaliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kupitia Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ambapo washiriki ni Wakuu wa Idara za Rasilimali Watu, Elimu (Msingi na Sekondari), Mifugo, Mipango, Katibu wa Afya, Maafisa Utumishi, Watendaji wa Kata (hawa ni kwa Halmashauri za Kilwa na Ruangwa ambazo zipo chini ya mradi). Halmashauri nyingine za Lindi, Manispaa ya Lindi, Liwale na Nachingwea wameshiriki Maafisa Utumishi.
Kaswa alisema kuwa lengo la warsha hii ni kuandaa mikakati ya kutoa motisha na vivutio kwa watumishi katika Halmashauri jambo litakalopelekea watumishi kuwa na motisha na tija katika kutekeleza mjukumu yao. Pamoja na hilo lengo kuu ni kuwafanya watumishi kushawishika kuendelea kubaki kwenye vituo vyao vya kutolea huduma hai itakayochangia katika upatikanaji wa huduma bora na endelevu kwa wananchi.
“Ni matarajio yangu kuwa jambo hili likifanikiwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakuwa na uwezo sio tu wa kuwabakisha watumishi wanaopangiwa bali pia kuinua kiwango cha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi katika sekta za elimu, afya, kilimo, mifugo, huduma za ardhi na maeneo mengine ya huduma”, alisema Kaswa.
Serikali ilishaona umuhimu wa jambo hili ndio maana ilipoandaa na kutunga Sera ya Malipo ya Mishahara na Motisha kwa Watumishi wa Umma ya mwaka 2011 suala hili la motisha lilibainishwa ikiwa ni pamoja na tafiti zilizofanyika ili kubaini maeneo yenye changamoto zaidi. Lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza zikiwemo uchache wa fedha na mwamko mdogo wa baadhi ya viongozi kwenye maeneo husika katika kutimiza majukumu yao ambazo zilisababisha mafanikio tarajiwa kutofikiwa.
Kaswa alisema kuwa serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza uboreshaji mazingira ya kazi kwa watumishi na ndio sababu ya uwepo wa warshaa hii ili kusifufua juhudi zilizokuwepo. Hii ni kutokana na watumishi baadhi wanaopangiwa kazi katika vituo mbalimbali kuacha kazi au wengine wanasingizia kuwa na matatizo ili wahame kutokana na changamoto wanazozikuta kwenye vituo vya kazi.
Pia ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la USAID kwa kuunga mkono jitihada hizi kama ambavyo wamekuwa wakiunga mkono katika maeneo mengine mengi ya maendeleo. Aidha, amewasihi washiriki kuhakikisha wanaandaa mikakati ya motisha kwa kuzingatia sababu zilizopelekea mikakati ya zamani kushindwa kufikia malengo yake. Vilevile amewasisitiza kuhakikisha katika mipango wanayoipanga wahakikishe kwanza ni ile inayotekelezeka ndani ya Halmshauri zao bila kusahau kubainisha wadau husika na namna watakavyoshiriki.
Serikali inaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali wanazokutana watumishi walio katika mazingira magumu kwa kadri uwezo unaporuhusu.
Aidha, tukumbuke kuwa suala la kutoa motisha kwa watumishi litakuwa na maana kama litakuwa ni endelevu, hivyo ni vema mipango mtakayotoka nayo hapa na kwengineko ijengwe ndani ya mifumo ya utendaji wa Halmashauri, ili iwe rasmi, endelevu na kuingizwa katika mifumo ya ufuatiliaji na uwajibikaji.
Mmoja wa waratibu wa mafunzo haya Bi. Restituta Masao ambaye alitoa maelezo mafupi kuhusu warsha hii alisema kuwa mpango mkakati huu utaandaliwa kwa kuzingatia hali ya kiutumishi na hali ya mazingira husika ili kuweza kuibua changamoto na kuzitafutia ufumbuzi. Pia alieleza kuwa katika mpango utakaoandaliwa utaainisha majukumu ya kila mdau kwani hii itasaidia katika usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mpango.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.