Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bi. Rehema Madenge pamoja na Katibu Tawala wa Lindi wa sasa Ndg. Ngusa Samike Wamefanya makabidhiano ya Ofisi ya Katibu Tawala ya Lindi. Makabidhiano yamefanyika leo asubuhi katika kikao kilichofanyika Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Lindi.
Akikabidhi ofisi hiyo leo jumanne mbele ya Wakuu wa Idara pamoja na Waandishi wa Habari, Bi. Rehema amemkaribisha Ndg. Samike mkoani Lindi kwa kumueleza jiografia ya mkoa pamoja na uwepo wa fursa mbalimbali adhimu. Ameeleza kuwa Mkoa wa Lindi umejaa madini takribani yote ikiwemo dhahabu, graphite isipokuwa Tanzanite na almasi, lakini kwa kiasi kikubwa madini yanayopatikana ni aina ya jasi ambayo yanachimbwa sana Wilayani Kilwa maeneo ya Kilanjelanje kwaajili ya uzalishaji wa saruji, gypsum powder viwandani.
Pamoja na uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi lakini bado matokeoya fursa hizo hayaakisi kwenye uchumi wa mkoa. “Lindi ni mkoa tajiri japo utajiri wake haujawa reflected sana na ndio kazi kubwa tunaendelea kufanya ili utajiri uliopo katika mkoa wa Lindi uonekane katika maisha ya watu……..kwa mfano kwenye korosho mpaka tunamaliza msimu tulifikia bilioni 142 lakini kwenye maisha ya wananchi huoni matokeo yake” ameeleza Bi. Madenge.
Bi. Madenge ameongeza kuwa ikiwa mkoa wa Lindi utatumia vizuri fursa za uchumi wa blue na vyanzo vya utalii kwa kutumia uwepo wa mbuga za wanyama, malikale , fukwe na bahari, Nyerere national park na serious game reserve inaweza kubadili hali ya maisha ya wananchi wa Lindi.
Kikubwa ambacho amesisitiza katika kuinua uchumi wa Lindi ni uimarishaji wa mawasiliano ambapo kwa sasa mawasiliano ya simu bado hayako vizuri kwenye maeneo mengi ya mkoa. Lakini pia miundombinu ya barabara za kuunganisha wilaya bado haiko vizuri hasa barabara za kwenda Liwale pamoja na maeneo ya Kilwa. Kufunguka kwa barabara nyingi za wilaya zitachochea maendeleo ya wananchi kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Lindi Ndg. Samike akimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini amesema kuwa ametoka mkoa wenye ziwa lakini amekuja kwenye mkoa wenye bahari hivyo suala kubwa ni utumiaji wa fursa za bahari ikiwemo ufugaji wa samaki kwenye vizimba kama ambavyo mwanza wanafanya.
Ndg. Samike ameahidi kutoa ushirikiano ili kuendeleza yale yote mazuri ambayo Bi. Madenge aliyaanzisha lakini akisisitiza kusimamia vizuri masuala ya mapato, kupunguza vifo vya wamama na watoto, vifo vya watoto wachanga, kusimamia masuala ya lishe, fedha zote za barabara matokeo yaonekane. Pia ameahidi kushirikiana vizuri na Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye ni mwenyeji ili aweze kupata uzoefu Zaidi.
Ikumbukwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya mabadiliko ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mkoa nchi nzima mwishoni mwa mwezi Julai 2022 ambapo kwa upande wa Lindi aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa Bi. Rehema Madenge amehamishiwa Mkoa wa Dar es salaam na aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg. Ngusa Samike amehamishiwa Mkoa wa Lindi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.