Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Ndg. Ngusa D. Samike amewataka wazazi, walezi na wanajamii kushirikiana katika kudhibiti matukio mbalimbali ya unyanyasaji kwa watoto ikiwemo ubakaji na ulawiti kwa watoto wa kiume ambayo hufanywa na watu wanaoaminika miongoni mwa wanajamii hao.
Katibu Tawala ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa- Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kwa muda wa robo ya kwanza iliyoanza mwezi Julai hadi Septemba 2022, kilichofanyika katika ukumbi wa mkutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi.
“Matishio ya malezi na makuzi ya mtoto yamezidi kuongezeka katika jamii zetu, na katika kipindi hiki cha watoto wengi hasa wa kiume ndio waliopo katika hatari zaidi za kufanyiwa vitendo hivi vya ukatili hususani matukio ya ulawiti, na watu wanaofanya matukio haya ni wale ambao jamii imekuwa ikiwaamini na kuwapa jukumu la kuwalea na kuwatunza watoto hawa ikiwemo ndugu wa karibu na muda mwingine viongozi wa dini ambao ndio tunawaamini sana”
Awali, akitoa taarifa ya robo mwaka ya Mkoa ya utekelezaji wa PJT-MMMAM, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Bwana. Gaudence Nyamwihura amesema mpango unajumuisha maeneo sita ambayo ni Afya, Elimu, Lishe, Ulinzi na Usalama, Malezi yenye Mwitikio na Uhamasishaji wa Programu ya PJT-MMMAM na unatekelezwa kwa kupitia ngazi za Halmashauri 6 za mkoa wa Lindi.
“Katika utekelezaji za afua za lishe, program imeongeza uhamasishaji wa wazazi na walezi kuchangia chakula mashuleni kwa madarasa ya awali na vituo vya kulelea watoto mchana katika kata nne za Halmashauri ya Liwale, ambapo katika kipindi cha Julai-Septemba 2022 jumla ya Tsh, 3,460,000 zilikusanywa na wananchi na kugharamia chakula cha mchana kwa watoto wa madarasa ya awali.”
Aidha, Bwana Nyamwihura ametoa pongezi kwa Halmashauri ya Kilwa kwa hatua za utekelezaji wa program hii ambapo tayari wameshaanza kutenga vifungu vya fedha kwa ajiri ya kuchangia chakula mashuleni na Halmashauri ya Manispaa ya lindi kwa kutoa elimu ya bustani ya mbogamboga na matunda kwa wanufaika wa TASAF ili kuhakikisha familia na watoto wao wanapata mlo kamili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.