Kayombo awataka watahiniwa kusoma kwa bidii
Katibu Tawala Msaidizi – Elimu, Ndg. Vicent Kayombo amewasihi watahiniwa wa kidato cha nne na cha sita kuhakikisha wanasoma kwa bidii.
Kayombo ameyasema hayo wakati alipotembelea sekondari ya Mbekenyera iliyopo wilayani Ruangwa kwa lengo la kuzungumza na watahiniwa wa kidato cha sita na che nne pamoja na walimu wao.
Katika mazungumzo hayo wanafunzi walihimizwa kuongeza jitihada katika kujisomea kwani hiyo ndio njia pekee ya kuwawezesha kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa iliyo mbele yao.
“Wote mnatambua kuwa mwaka huu mtatakiwa kufanya mitihani ya taifa, hivyo niwasihi kuongeza jitihada katika kujisomea na pale ambapo mtaona hamuelewi msisite kuwafuata walimu wenu ili waweze kuwaelekeza zaidi”, alisema Ndg. Kayombo.
Katika ziara hiyo aliwasihi walimu kuhakikisha wanaongeza kasi katika ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi kwani kwa mwaka huu ufaulu ni lazima uongezeke katika mkoa. Pia alisisitiza mambo yafuatayo:-
Amewataka walimu kuongeza kushirikiano katika utendaji kazi wa kila siku.
Walimu kuzungumza na watahiniwa mara kwa mara na kutambua uwezo wao ikiwa ni pamoja na kuwapanga kwenye makundi kila wanapofanya mitihani na kuhakikisha wanaendelea kuongeza ufaulu.
Amewasihi watumishi wa elimu kukosoana kwa wale ambao hawatimizi wajibu wao bila kuoneana aibu kwa kuonyesha mapungufu mtumishi aliyonayo.
Pia aliwataka maafisa elimu kata kuhakikisha wanasimamia maendeleo ya elimu katika kata zao kwa kuhakikisha wanatembelea na kukagua shule mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kuingia madarasani.
Timu za Ufuatiliaji zinazofika Shuleni, zihakikishe changamoto zote za ufundishaji zinazotolewa na walimu au ujifunzaji zinazotolewa na wanafunzi zinapata ufumbuzi na zile zinazohitaji kufika mamlaka za juu basi zifikishwe kwa haraka.
Aidha, Kayombo aliwapongeza walimu na maafisa elimu kata kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya ufundishaji na usimamizi wa maendelep ya elimu kwa ujumla ambapo pia aliwasihi kutokata tamaa bali wazidi kuongeza jitihada ili wanafunzi wa mkoa wa Lindi waweze kupata matokeo mazuri.
Pia ameupongeza uongozi wa wilaya ya Ruangwa kwa namna wanavyoshirikiana katika kusimamia elimu ndani ya wilaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.