Kiongozi wa Mbio za Mwenge Ndg. Abdalla Shaib Kaim amewapongeza Viongozi wa Wilaya ya Ruangwa kwa kazi nzuri ya Usimamizi wa Miradi.
Ndg. Kaim ametoa pongezi hizo jana Jumatano wakati Mwenge wa Uhuru ulipofika na kukagua jumla ya miradi 7 ya maendeleo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 2.4 katika Wilaya ya Ruangwa.
Akifungua barabara yenye urefu wa 1.051 ya NHC iliyojengwa katika kata ya Nachingwea kwa kiwango cha lami kwa thamani ya fedha Tsh. 562,196,293.33 , Ndg. Kaim amesema kuwa viongozi wa Wilaya ya Ruangwa wameonesha umahili mkubwa katika kusimamia miradi ya maendeleo.
Ndg. Kaim ameongeza kuwa ubora wa miradi unatokana na uongozi imara unaosimamia utekelezaji wa Miradi hiyo. Ametoa pongezi kwa Wakala wa Barabara, Vijijini TARURA kwa ubora mzuri wa Miradi wanayoisimamia.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Hassan Ngoma amesema kuwa pamoja na uongozi mzuri wa Wilaya lakini usimamizi mzuri wa miradi unatokana na ushirikishwaji dhabiti wa wananchi katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mhe. Ngoma amezungumza hayo mbele ya Kiongozi wa mbio za Mwenge pamoja na wananchi katika zoezi la uwekaji jiwe la msingi kwenye jengo la OPD, Maabara na Kichomea taka katika Kituo cha Afya Namichiga iliyopo kijiji cha Namichiga B, Wilaya ya Ruangwa.
Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Ruangwa umekimbizwa jumla ya kilomita 118 na kuweka mawe ya msingi katika Kituo cha Afya Namichiga, mabweni mawili ya Shule ya Sekondari Lucas Malia iliyopo kijiji cha Ng'au pamoja na mradi wa upanuzi wa skimu ya maji Mandawa.
Pia umetembelea jumla ya shughuli na miradi 6 ikiwemo mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, mradi wa lishe, mapambano dhidi ya rushwa, uhifadhi wa chanzo cha maji na mazingira, pamoja na mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI na Malaria.
Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Ruangwa zimehitimishwa jana Jumatano ambapo leo alhamisi Wilaya ya Lindi imekabidhiwa Mwenge kuukimbiza katika Manispaa ya Lindi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.