Kituo cha afya Narungombe kilichopo katika Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kinatarajiwa kuanza kutoa huduma za afya kwa wagonjwa wa nje (OPD) kuanzia Oktoba 1, 2022 baada ya kukamilisha kikamilifu ujenzi wa majengo matatu ya awali ambayo yanajumuisha sehemu ya wagonjwa wa nje, maabara na kichomea taka.
Gladness Mwaindosa, Mganga mfawidhi katika zahanati ya Narungombe ameeleza kuwa kufunguliwa kwa kituo hiko cha afya kunaenda kuleta afueni ya upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wapatano 3500 waliopo katika kata ya Narungombe ambao kwa muda mrefu walikua wanapata huduma za afya katika zahanati iliyopo katika eneo hilo na muda mwingine walipaswa kusafiri hadi Ruangwa kupata huduma hizo.
“Kwa mwanzoni watu walikua wanapata shida sana hasa kukiwa na mama mjamzito sababu inabd gadi mpate msaada wa gari ili akapate huduma ya kujifungua Ruangwa, lakini kwa sasa hivi tunashukuru kwakua kituo chetu kikikamilika kabisa tutakua na huduma zote hapa ikiwemo huduma za upasuaji. Hakutakua tena na ulazima wa mtu kuingia gharama za kusafiri kutoka hapa kwenda Ruangwa”ameongeza.
Naye, bwana Omary Rajabu , mwananchi na mkazi wa Narungombe ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya umeweza kwanza kumnufaisha yeye binafsi kama mkazi wa kata hiyo kwa kumpatia ajira.
“Mradi huu umeninufaisha mimi binafsi kama fundi kwa kunipa ajira na kuniongezea kipato, kama tujuavyo sasa hivi ajira zimekuwa ngumu hivyo uwepo wa mradi huu umenifanya mimi kupata ajira hapa ya ujenzi ambao umenifanya nipate kipato mimi na wenzangu ambao wengine pia sio wakazi wa hapa lakini wote tunafanya kazi hapa na tunapata pesa ya kuendeshea maisha yetu.” Ameeleza.
Katibu Tawala mkoa wa Lindi, Ndg. Ngusa Samike ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Ruangwa kwa usimamizi thabiti wa kituo hiko cha afya na kuagiza kuendelea kwa kasi hiyo katika majengo mengine mapya ambayo yameongezewa ikiwemo Jengo ya upasuaji, wodi za wagonjwa na jengo la kufulia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.