Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack Jana Jumanne ameongoza Kamati ya Usalama Mkoa na Wilaya, Askari wa uhifadhi wa Nyerere wakiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo Kamishna Witinnes Shoo kufanya doria ya kuwaondoa wafugaji waliovamia hifadhi ya Taifa ya Nyerere, katika eneo la Wilaya ya Liwale.
Mhe. Telack amefanya operasheni hiyo ikiwa ni muendelezo wa kuhakikisha hifadhi zote za Serikali zinabaki salama.
Katika oparesheni hiyo, Mhe. Telack amemtaka Ndg. Ntalimbo mmiliki wa ng'ombe 547, punda 11 na ndama 3 walioshikiliwa na Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ajitokeze ili alipe faini ya kuingiza ng'ombe wake kwenye hifadhi. Kwa mujibu wa Afisa Uhifadhi Julius Shija tarehe 29 Januari 2023 Askari wa kituo cha Liwale waliwakamata jumla ya ng'ombe 547 na punda 11 wakiwa ndani ya Hifadhi ya Nyerere. Pia walikamatwa watuhumiwa wawili wakichunga mifugo hiyo ndani ya hifadhi waliojulikana kwa majina John Lucas na Simbi Masingija.Baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kufuata taratibu za Polisi, mnamo tarehe 01/02/2023 shauri la mashtaka lilifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Liwale. Shauri hilo lilisikilizwa na mashahidi wawili walitoa ushahidi kisha Mahakama ilihamia eneo la tukio (ndani ya hifadhi) kwa ajili ya kupokea kielelezo ambacho ni ng'ombe 547 na punda 11.
Afisa Uhifadhi Shija ameendelea kuieleza kamati ya Usalama kuwa, pamoja na kujiridhisha kwa kutembelea eneo la tukio na kuwasikiliza mashahidi, baada ya kuwapa nafasi ya kujitetea tarehe 10/02/2023 majira ya saa 09:20 Mahakama iliwaachia huru watuhumiwa na kuamriwa warudishiwe mifugo yao kutokana na ushahidi upande wa serikali kutojitosheleza. Muhifadhi Shija anasema,
Mhe. Telack akionesha kusikitishwa na maamuzi ya Mahakama ya Wilaya kumuachia huru mmiliki huyo wa mifugo licha ya Hakimu kujiridhisha kwa kufika eneo walipokamatwa mifugo hiyo ambapo baada ya hukumu hiyo Serikali imekata rufaa. Ameongeza kuwa wakati rufaa ya kesi hiyo ikisubiriwa, mmiliki huyo alipe faini kuingiza mifugo hiyo kwenye hifadhi ili akabidhiwe mifugo hiyo.
" Kwa sababu amekwenda kwa Mkuu wa Wilaya na akakili kwamba ng'ombe wake wapo kwenye hifadhi na akaomba msaada kwa Mkuu wa Wilaya kwamba asaidiwe alipe faini, nataka atoke huko alipo arudi kwa Mkuu wa Wilaya alipe faini na achukue ng'ombe wake".
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Liwale Mhe. Goodluck Mlinga amesema kuwa mifugo imekuwa changamoto kubwa kutokana na tabia ya wafugaji hao kuingiza mifugo ya kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na kulisha mazao ya wakulima.
Ameongeza kuwa ataendelea kuchukua hatua Kali dhidi ya wafugaji wasiofuata Sheria na taratibu.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa na timu yake baada ya kukutwa kwenye eneo la hifadhi akiishi na familia yake mfugaji mwingine Ndg. Mnyama Masasa ambaye ni mfugaji wa kisukuma amesema kuwa yeye hakufahamu kama yumo ndani ya hifadhi kwa muda wote alioshi hapo. Baada ya kupewa ufafanuzi juu mipaka ya hifadhi, mfugaji huyo na wenzake wameahidi kuondoa mifugo yao ndani ya hifadhi.
Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ndio eneo linalojengwa bwawa kubwa kwa ajili ya kuzalisha umeme, nishati ambayo ndio kiini cha uzalishaji. Hifadhi hii kwa manufaa yake kitaifa haina budi ilindwe kwa kuzuia uvamizi wa aina yoyote unaohatarisha mazingira ya hifadhi ki ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.