Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Ndg. Ngusa Samike Leo Jumatatu amezindua zoezi la ugawaji wa pikipiki zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo.
Akizindua ugawaji wa pikipiki 291 zilizotolewa kwa Maafisa Kilimo wa Mkoa wa Lindi, Ndg. Ngusa Samike amewataka Maafisa Kilimo kuzitumia pikipiki hizo kwa shughuli ya kuihudumia jamii na si vyinginevyo. Amesisitiza kuwa upatikanaji wa pikipiki hizo uendane na matokeo chanya kwenye sekta ya Kilimo.
Ndg. Ngusa amewaasa pia Maafisa hao kutumia pikipiki hizo kwa umakini na tahadhali ili kujilinda na ajali ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya wataalam wa Serikali.
Awali Akizungumza mbele ya Maafisa Kilimo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Ndg. Barnabasi Esau amewasihi Maafisa hao kuzitunza na kuzihudumia pikipiki hizo ili zidumu na kuleta tija.
Akisoma taarifa ya ugawaji wa pikipiki hizo, Ndg. Majid Myao amesema kuwa awamu ya kwanza Mkoa wa Lindi ulipokea pikipiki 6, awamu ya pili Mkoa ulipokea pikipiki 23 na awamu ya tatu Mkoa umepokea pikipiki 262 na kufanya idadi ya pikipiki zilizotolewa kwa Mkoa kufikia 291 ambazo pikipiki 3 zimetolewa kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na jumla ya pikipiki 288 zimepelekwa kwa Maafisa Kilimo na Maafisa Ushirika.
Akizungumza kwa niaba ya Maafisa ugani, Bi. Amina Pemba ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutatua changamoto ya Maafisa ugani katika utoaji wa huduma kwa wakulima. Amesema kuwa kwa sasa wakulima watapata huduma kwa wakati Kwa kuwa uwezo wa kuwafikia umeimarishwa.
Pikipiki hizo zinatolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya kiongozi mahili Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mwendelezo wa kuimarisha mazingira ya wataalam wake katika kuwahudumia wananchi kwa wakati na uhakika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.