Maandalizi ya Tamasha la Utamaduni wa Jamii ya Lindi yaanza
Wadau wa utamaduni katika mkoa wa Lindi wamefanya kikao chao cha kwanza cha maandalizi ya tamasha la utamaduni wa jamii ya Lindi litakalofanyika katika Kijiji cha Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam.
Kikao hiki kiliongonzwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi na wajumbe wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Mkurugenzi Msaidizi wa Makumbusho ya Taifa, Bi. Agnes, Meneja wa TFS, Bi. Debora Mwakanosya, Wakuu wa Taasisi na Mashirika mbalimbali wa Mkoa wa Lindi, Mwenyekiti wa KAUJALI, Ndg. Abdalla Hanga, Maafisa Utamaduni, Viongozi wa vikundi vya Sanaa, na wataalam mbalimbali.
Bi Agnes aliwaeleza wadau mipango na namna tamasha hilo litakavyokuwa ambapo alisema kuwa tamasha litakuwa ni la siku nne. Siku ya kwanza kutakuwa na ufunguzi utakaoambatana na uzinduzi wa nyumba ya utamaduni wa jamii ya Lindi inayotarajiwa kujengwa katika eneo la makumbusho ya taifa.
Siku ya pili kutakuwa na kusomeana hadithi na simulizi mbalimbali kuhusiana na jamii za mkoa wa Lindi ambapo watu watapata nafasi kusikia kutoka kwa wazee mbalimbali watakaochaguliwa katika kusimulia historia za makabila na vitu mbalimbali. Siku ya tatu na ya nne viongozi na wadau mbalimbali watapata fursa ya kuzungumzia kuhusu maendeleo ya mkoa wa Lindi kuanzia mkoa ulipoanzishwa, ulipo na unapoelekea.
Naye Bi. Mwakanosya aliwaeleze wadau kuhusu fursa zilizopo katika utalii wa utamaduni na namna mkoa unavyotakiwa kujipanga kuonyesha utalii huo katika tamasha.
Mhe. Zambi aliwataka wajumbe wote kuhakikisha wanajipanga vizuri kuhakikisha tamasha hilo linafanyika kwa ubora unaostahili hasa ukichukulia mkoa wa Lindi ndio unaozindua kijiji kipya cha makumbusho ya taifa. Pia wakuu wa wilaya kuhakikisha wanakwenda kufanya uhamasishaji wa kutosha ili wananchi wengi waweze kutambua uwepo wa tamasha hilo ili wale watakaokuwa na uwezo waweze kushiriki.
Aidha, Mhe. Zambi amezitaka kamati zilizoundwa kukutana mara moja na kuanza kujipanga ni namna gani mkoa utalifanikisha tamasha hili kwani muda uliobakia ni mdogo sana. Wananchi wamehimizwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika tamasha hilo kwani licha ya kuonyesha masuala ya kiutamaduni pia watapata fursa ya kibiashara kwa kuonyesha bidhaa mbalimbali wanazotengeneza na kuziuza.
Tamasha la utamaduni wa jamii ya mkoa wa Lindi litafanyika tarehe 26 – 29 September, 2018 ambapo litaambatana na uzinduzi wa nyumba ya asili ya watu wa lindi itakayojengwa kijijini hapo. Kwa sasa kijiji cha makumbusho kinaanza kujengwa upya kwa kufuata ramani ya Tanzania, hivyo kila mkoa utatakiwa kuwa na nyumba ya asili ya mkoa husika kulingana na ramani ya Tanzania.
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao cha maandalizi ya tamasha la utamaduni mkoa wa Lindi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.