Kambi ya Madaktari Bingwa na Ubingwa Bobezi wa Rais Samia inayoendelea katika mkoa wa Lindi imeokoa maisha ya mama mjamzito ambaye mimba yake ilitungwa nje ya mji wa mimba kwa kumfanyia upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa.
Upasuaji huo umefanyika Septemba 17, 2024 katika Hospitali ya Wilaya Ruangwa ukiongozwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake uzazi na Watoto Dkt. Lilian Mnabwiru kwa mgonjwa aliewasili hospitalini hapo akiwa katika hali ya hatari na kuhitaji kufanyiwa upasuaji wa Dharura.
“Kuna mama ambae alikuwa anatokwa damu ndani kwa ndani kwasababu mimba yake ilitungwa nje ya mji wa mimba tulimkuta katika hali mbaya kwani damu nyingi ilikuwa imepotea pressure imeshuka na hivyo alikuwa katika hali mbaya sana.” Amesema Dkt. Mnabwiru
Dkt. Mnabwiru ameendelea kusema kuwa mimba kutungwa nje ya mji wa mimba ni hatari kwa mama na mtoto kwani mtoto atakosa mahitaji muhimu katika ukuaji wake lakini walifanikiwa kuondoa kiumbe kilichojipandikia na kuzuia damu iliyokuwa inavuja ndani ya tumbo.
“Tulitoa damu takribani lita mbili na nusu zilizovujia tumboni na kumuongezea damu nyingine kurudisha ile iliyopotea. Mgonjwa ameshaamka na anaendelea vizuri kwa sasa.” Amesema Dkt. Mnabwiru
Kwa upande wake, Bi Maua Ally ambaye ni mdogo wa mgonjwa huyo amewashukuru Madaktari bingwa wa Rais Samia kwa kuokoa maisha ya dada yake kwani hali yake ilikuwa mbaya sana lakini kwa jitihada zao zimerejesha matumaini kwa Mgonjwa.
“Mgonjwa alipoteza fahamu kabisa lakini tulivyofika hapa tumekutana na maktari bingwa wamemuhudumia na sasa haliyake imeimarika.” Amesema Bi. Maua
Kambi hii ya Matibabu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia inaendelea Mkoani lindi katika Hospitali zote za Wilaya hivyo wananchi wanahimizwa kwenda Hospitalini kwani huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi zimesogezwa karibu kwa lengo la kupunguza gharama kubwa za kufuata Huduma hizo kwenye Hospitali za Kanda na Rufaa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.