Katika kusheherekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mh. Bi Zainab Telack amewataka wananchi kujivunia mafanikio yaliyopatikana katika mkoa na kuipongeza serikali kwa jitihada mbalimbali za maendeleo zilizofanyika tangu nchi ipate uhuru.
Mkuu wa mkoa ameyasema hayo katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kimkoa katika halmashauri ya wilaya ya Liwale, Uwanja wa michezo ambapo amesema serikali imejitahidi kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara kwa viwango vya lami pamoja na usimamizi mzuri uliowekwa na serikali katika kuhakikisha wakulima wa mazao ya korosho na ufuta hawakumbani na changamoto zozote katika kilimo.
‘‘Kwa mwaka 2019 pekee, sh. bilioni 167 zimepatikana katika mauzo ya korosho huku zao la ufuta likiingiza sh. bilioni 123 hivyo usimamizi mzuri wa mauzo katika mazao haya ya biashara yamefanya kuongezeka kwa kipato cha wananchi wa Lindi vilevile mapato ya halmashauri zote za Mkoa wa Lindi, hivyo tuna mengi mazuri ya kujivunia sisi kama mkoa katika miaka 60 ya Uhuru’’
Katika sekta ya elimu Mh. Telack amesema ‘‘ Kipekee naomba niipongeze serikali yangu ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha zaidi ya sh. Bilioni 8.1 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vya kisasa 401 na bweni moja ili kila mwanafunzi na mwalimu awe katika mazingira rafiki ya kujifunza, kujifunzia na kufundisha’’
Aidha, katika sekta ya maji Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa mkoa wa Lindi unaadhimisha miaka 60 ya Uhuru kwa kuendeleza kampeni ya kumtuma mama ndoo kichwani ambapo mkoa umefanikisha upatikanaji wa maji katika maeneo ya mijini kwa asilimia 76 na vijijini kwa asilimia 68.75.
‘‘Serikali yetu chini ya uongozi wa rais Samia Suluhu inakamilisha ununuzi wa magari ya kuchimba visima ambavyo vitatumika na hapa kwetu Lindi ili tuweze kutatua kero na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa maji hasa katika maeneo ya vijijini’’ ameongeza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.