Manispaa ya Lindi yatakiwa kuboresha uwanja wa Ilulu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Manispaa ya Lindi kufanya ukarabati katika uwanja wa michezo wa Ilulu.
Maagizo haya ameyatoa wakati alipotembelea uwanja wa michezo wa Ilulu kwa lengo la kuona hali ya uwanja ilivyo kwa sasa. Uwanja wa Ilulu ulijengwa mwaka 1957, na toka kipindi hicho uwanja umekuwa ukifanyiwa ukarabati mdogo lakini kwa sasa unatakiwa kufanyika ukarabati mkubwa.
Mhe. Majaliwa alisema uwanja wa Ilulu unatakiwa kufanyiwa ukarabati kwani ndio uwanja unaotakiwa kutumika kwa shughuli mbalimbali za mkoa kwa kuwa upo katika makao makuu ya mkoa. Ambapo kwa mwaka 2019 mkoa wa Lindi utakuwa mwenyeji wa maadhimisho kilele cha mbio za mwenge wa uhuru, kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na wiki ya vijana. Pia mashindano ya taifa cup 2019 yanatarajiwa kufanyika katika mkoa wa Lindi..
“Mkoa wa Lindi umachaguliwa kuwa ndio utakaoadhimisha kilele cha mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2019, pia TFF wamenieleza kuwa wanataka mashindano ya taifa cup 2019 yafanyike mkoani Lindi. Kutokana na umuhimu wa matukio hayo naiagiza manispaa ya Lindi kuhakikisha wanaufanyia ukarabati uwanja huu kwa kujenga makujukwaa, vyoo, nyasi, fensi ndogo ya sehemu ya kuchezea mpira na kuuboresha ukuta unaozunguka uwanja”, alisema Mhe. Majaliwa.
Uwanja wa Ilulu kwa sasa una majukwaa matatu (3) ambapo kuna jukwaa kuu na majukwaa mengine 2 ambayo yote yamejengwa katika upande mmoja. Mhe. Majaliwa ameiagiza manispaa kuongeza majukwaa mengine mawili (2) kwenye upande mwingine wa uwanja ili kila upande uweze kuwa na majukwaa.
Mkurugenzi wa manispaa ya Lindi, Jomaary Satura amesema kuwa manispaa imeyapokea maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu na kuahidi kuwa manispaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itajipanga kuhakikisha uwanja unafanyiwa ukarabati na kukamilika kabla ya Septemba, 2019.
Nao wananchi wa manispaa ya Lindi wamempongeza Mhe. Waziri Mkuu kwa kutoa maagizo ya ukarabati wa uwanja wa Ilulu kwani ni muda mrefu uwanja huo haujafanyiwa ukarabati mkubwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.