Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, ameongoza kikao cha kwanza cha maandalizi ya Maonesho ya Madini kimkoa kilichofanyika leo Aprili 4, 2025, katika ukumbi wa hoteli ya Ruangwa Pride, wilayani Ruangwa huku aitaja juni 11 hadi 14 , 2025 kuwa tarehe rasmi ya kufanyika kwa maonesho ya madini ya Mkoa wa Lindi.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji, wakuu wa vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa (RS), Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri na Manispaa, wakuu wa taasisi mbalimbali pamoja na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama kwa lengo la kupanga kwa pamoja maandalizi ya maonesho hayo.
Aidha, Mhe. Telack ameeleza kuwa maandalizi hayo ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha maonesho yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya madini vilivyopo wilayani Ruangwa mkoani Lindi yanakuwa na mafanikio makubwa, huku akisisitiza ushirikiano wa pamoja kutoka kwa wadau wote.
“Maonesho haya ni fursa muhimu ya kuonesha rasilimali zetu za madini, kuwavutia wawekezaji na kuinua uchumi wa wananchi wetu, ni wajibu wa kila mdau kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha tunapata mafanikio tunayoyatarajia,” amesema Mhe. Telack.
Kwa upande wao, Wadau wa madini wameeleza utayari wao kushiriki kikamilifu katika maandalizi hayo, huku wakiahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali ili kufanikisha maonesho hayo ambayo yanatarajiwa kuinua uchumi wa wachimbaji na Mkoa kwa ujumla.
Maonesho ya madini Mkoa wa Lindi yanatarajiwa kufanyika tarehe 11 - 14 Juni, 2025, yakiwakutanisha wachimbaji, wawekezaji na taasisi za kifedha, kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kuonesha teknolojia mpya pamoja na kukuza fursa za uwekezaji katika sekta ya madini, ambapo mwaka huu kunatarajiwa kufanyika mnada mkubwa wa madini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.