Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022, idadi ya watu katika Mkoa wa Lindi imeongezeka kutoka watu 864,652 hadi kufikia watu 1,194,028 katika kipindi cha miaka 10 tangu 2012. Sawa na ongezeko la idadi ya watu 329,376.
Matokeo hayo yameelezwa jana kupitia taarifa ya Wiziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa iliyosomwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye kwenye mkutano wa Uwasilishaji na Uhamasishaji wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa Viongozi, watendaji na wadau wa ngazi mbalimbali katika mkoa wa Lindi uliofanyika jana tarehe 21 Februari 2024 katika kiwanja cha mpira wa miguu cha Ilulu, Manispaa ya Lindi.
Kupitia taarifa hiyo, Mhe. Majaliwa amesema kuwa Kati ya watu 1,194,028 waliopo Mkoani Lindi, idadi ya wanawake ni 611,908 na idadi ya wanaume ni 582,120 ikionesha kuwa idadi ya wanawake ni wengi zaidi ya wanaume.
Aidha, Kwa Mkoa mzima, Wilaya ya Kilwa inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ambayo ni 297,676 sawa na asilimia 25(robo ya idadi ya wananchi wote wa Mkoa). Wilaya ya Liwale ina idadi ndogo zaidi ya watu ambayo ni 136,505 ukilinganisha na Wilaya zote za Mkoa wa Lindi.
Kasi ya ongezeko la idadi ya watu katika Mkoa wa Lindi ilikuwa ni asilimia 0.9 mwaka 2012 huku ikiongezeka mpaka kufikia asilimia 3.2 kwa mwaka 2022.
Mhe. Majaliwa amewataka wananchi wote kutafakali kwa kina juu ya Kasi ya ongezeko la idadi ya watu ukilinganisha na kasi ya maendeleo ya mkoa.
Ameongeza kuwa matokeo ya Sensa yatatuwezesha kujipima, kujitathimini mahali tulipo na kuweka mipango ya kimkakati ya kuchochea kasi ya maendeleo kwa mkoa wa Lindi na Taifa kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.