Kamati ya Mawaziri wa Kisekta imewasilisha Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 na kupiga marufuku ufanyaji za shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi ya msitu wa Nyengedi na Pori la Akiba la Selous mkoani Lindi.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha Mawaziri wa Kisekta na wataalamu wa mkoa, mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe Dkt. Angelina Mabula, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema
“Hivi vijiji vina maeneo ya kutosha katika vijiji vyao lakini chakushangaza ni kwamba hawaridhiki na maeneo waliyonayo hawajaweza kuyalima yote na kuyamaliza na bado wanaingia katika hifadhi wanafanya kilimo na kurudi kijijini, sasa kuanzia leo Mhe Mkuu wa Mkoa vijiji hivyo haviruhusiwi kuingia kwenye maeneo ya hifadhi na kufanya shughuli zao za kilimo, wanaharibu vyanzo vya maji na ekolojia nzima ya viumbe na maeneo yetu,kuna vijiji viwili vyenyewe vitabaki ndani ya hifadhi na vitabaki na hadhi yake kwasababu tayari havina migogoro katika maeneo hayo”
Aidha, Dkt Mabula amevitaja vijiji hivyo kuwa ni Chiodya A na Chiodya B, Mihango, Mtauna, Mnara na Mkanga ambavyo vinapakana na hifadhi ya msitu wa Nyengedi pamoja na vijiji vya Zinga Kibaoni, Mtepera na Kikulyungu ambavyo vinapakana na Pori la Akiba la Selous.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe Zainab Telack amewataka wakulima kuacha kilimo cha kuhamahama na wafugaji kutumia kikamilifu maeneo waliyotengewa “ Sisi kama mkoa tulishatenga maeneo maalumu ya wafugaji kwa ajiri ya kufanya shughuli zao za ufugaji katika kila halmashauri na tulishaanza mchakato wa ujenzi wa marambo kwa ajiri ya kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa mifugo hasa kipindi cha kiangazi, tumeendelea pia kuhamasisha wananchi wetu kulima katika mashamba ambayo tayari wanayo ili kuepusha hii migogoro ya ardhi na uvamizi katika hifadhi”
“Bado kuna ardhi ya kutosha katika vijiji vyetu, ardhi ambayo bado ni mpya na nzuri inafaa kwa kilimo kwakweli hatuna sababu ya kugombea ardhi kwasababu bado tunayo ipo ya kutosha” ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.