Mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Nanjilinji A na Kijiji cha Mirui kutatuliwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amesema amekuja Lindi na majibu ya utatuzi wa mgogoro wa mpaka wa kijiji cha Nanjilinji A na Kijiji cha Mirui.
Mhe. Lukuvi ameyasema hayo leo kabla ya kuanza kikao kilichowajumuisha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya za Kilwa na Liwale. Pia katika kikoa hicho walishiriki Wakuu wa Wilaya za Lindi na Ruangwa pamoja na wataalam toka wizara ya ardhi, mkoa na halmashauri za wilaya husika.
“Leo tumekuja na majibu ya mgogoro wa mpaka uliopo kati ya Kijiji cha Nanjilinji A kilichopo Wilaya ya Kilwa na Kijiji cha Mirui kilichopo Wilaya ya Liwale baada ya timu ya Wataalam kupitia nyaraka mbalimbali zilizotumika katika uanzishwaji wa Wilaya na Vijiji hivyo”, alisema Mhe. Lukuvi.
“Licha ya kutatua mgogoro huo, wizara kwa kushirikiana na mkoa na wilaya watapima na kuweka alama za kudumu (mawe) za mipaka katika vijiji hivyo ikiwa ni pamoja na kuwatengenezea mpango wa matumizi bora ya ardhi”, aliongeza Mhe. Lukuvi.
Aidha, Mhe. Lukuvi amesema kuwa wizara imejipanga kuhakikisha inaboresha ofisi zake za kanda ambapo kwa kanda ya kusini maafisa wote muhimu wameshapelekwa na vifaa vya kazi vitawasili mwezi Agost, 2018. Hivyo shughuli nyingi zinazohusu masuala ya ardhi zitakuwa zinamalizika katika ofisi za kanda na sio wizarani kama ilivyokuwa awali.
Kutokana na maboresho hayo ya ofisi za kanda, Mhe. Lukuvi amesema kwamba wizara inatarajia kwamba halmashauri katika kanda husika zitahakikisha vijiji vyote vinapimwa, mpango wa matumizi bora wa vijiji unaandaliwa na wananchi wenye ardhi wanamilikishwa kwa kupatiwa hati.
Mhe. Lukuvi amepongeza jitihada zinazofanywa na mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Godfrey Zambi za kuhakikisha migogoro ya ardhi iliyopo inatatuliwa, na kwamba ni imani yake kuwa Mkoa unaweza kumaliza migogoro iliyopo kabla ya muda uliowekwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi akimkaribisha waziri lukuvi , alisema mkoa unaendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kumaliza migogoro ya ardhi iliyopo. Ambapo pia alitaja baadhi ya migogoro hiyo kuwa ni wananchi kuvamia shamba la Mauhumbika (Mahumbika Plantation), Shamba la Mkwaya katika Wilaya ya Lindi, mgogoro wa mpaka kati ya wananchi na Kikosi namba 843 jeshi la wananchi JWT na Kikosi 41 JKT vya jeshi la kujenga taifa ambavyo vipo katika Wilaya ya Nachingwea.
Vilevile aliuelezea mgogoro wa mpaka uliopo wa kijiji cha Nanjilinji A – Kilwa na kijiji cha Mirui – Liwale. Migogoro mingine iliyopo sio mikubwa sana ambapo mkoa kwa kushirikiana na wilaya imekuwa ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuitatua.
Mhe. Zambi amempongeza waziri kwa kazi nzuri anayoifanya katika wizara hasa katika kutatua migogoro ya ardhi iliyopo pamoja na kuongeza wataalam katika ofisi za kanda ili kusogeza upatikanaji wa huduma za masuala ya ardhi jirani na wananchi.
Mhe. Lukuvi licha ya kufanya mkutano na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama, pia mchana atasikiliza malalamiko ya masuala ya ardhi toka kwa wananchi wa manispaa ya Lindi na maeneo ya jirani na kuyatolea ufumbuzi. Aidha, kesho tarehe 10 Julai, 2018 atakwenda katika Kijiji cha Mirui na Kijiji cha Nanjilinji A ambapo katika maeneo yote hayo atazungumza na wananchi kuwaelezea hali halisi ya mipaka ilivyo na mpango uliopo katika kumaliza mgogoro uliopo.
BAADHI YA PICHA ZA VIKAO ALIVYOFANYA MHE. LUKUVI.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.