Mhe. Aweso asikitishwa na Mradi wa Maji wa Ng’apa
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesikitishwa na kutokamilishwa kwa mradi wa maji wa Ng’apa kwa mujibu wa mkataba.
Mhe. Aweso alifanya ziara mkoani Lindi kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi wa maji wa Ng’apa uliopo katika Manispaa ya Lindi na kujikuta akisikitishwa na kasi ya mkandarasi kushindwa kukamilisha asilimia 10 ya kazi zilizobakia.
“Kwa kweli leo nimesikitishwa na kuumizwa sana kuona mradi huu wenye ufadhilli mkubwa wa zaidi ya Euro milioni 13 ambao fedha zake zipo lakini mkandarasi amechukua muda mrefu kuutekeleza na mpaka sasa anashindwa kukamilisha asilimia 10 zilizobaki ili mradi ukamilike”, alisema Mhe. Aweso.
“Lengo la serikali ya chama cha mapinduzi ni kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanapata maji safi, salama na yenye kujitosheleza kwa asilimia 85, na asilimia 95 kwa wanaoishi mijini”, aliongeza Mhe. Aweso.
Aidha, Mhe. Aweso aliwaahidi viongozi wa Lindi kuwa akaporudi Dodoma atafanya kikao cha dharura na viongozi wa wizara ili kuona ni nini kinasababisha mradi huo usikamilike kwa wakati. Pia wataangalia njia sahihi za kuvunja mkataba na mkandarasi ili kazi zilizobakia ziweze kukamilishwa na wataalam wa wizara.
Mhandisi mshauri wa mradi kutoka kampuni ya KFW Consultant, Ndg. Audax Rweyemamu alisema kuwa wameshatoa ushauri mara mbili kwa wizara ili ivunje mkataba na mkandarasi kutokana na kuonekana kushindwa kumaliza kazi iliyobakia ya asilimia kumi kwa wakati lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Lindi. Mhe. Shaibu Ndemanga alieleza kuwa ni faraja sana kuona kwamba serikali itaenda kuchukua hatua za mwisho kuhakikisha kuwa mkandarasi mkataba wake unasitishwa kutokana na ucheleweshwaji wa mradi huo uliotakiwa kukamilika toka mwaka 2015. Kwa maamuzi hayo wizara kupitia wataalam wake wataweza kukamilisha mradi kwa wakati na wananchi wa Lindi watapata maji safi na salama.
Aidha, amepongeza jitihada zinazofanywa na serikali kupitia wizara ya maji katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata maji safi na salama.
Mhe. Aweso alisomewa taarifa ya hali ya huduma ya maji na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Ndg. Majid Myao ambapo alimuelezea hali utekelezaji wa miradi ya maji katika mkoa, hali ya upatikanaji wa maji safi na salama ambapo kwa upande wa vijijini jumla ya wakazi 413,503 sawa na asilimia 54.9 kati ya wakazi wapatao 864,652 (kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012) wanapata huduma ya maji safi na salama.
Kwa upande wa Manispaa ya Lindi idadi ya watu wanaopata huduma ya Maji safi na salama ni watu wasiopungua 68,976 sawa na asilimia 75% ya wakazi wote. Na katika miji ya Wilaya wastani wa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni 67.96%.
Mradi wa maji wa Ng’apa upo katika Manispaa ya Lindi na umekuwa ukitekelezwa tangu mwaka 2013 ambapo mpaka Agosti, 2018 utekelezaji wa mradi huu ulikuwa umefikia asilimia 90. Mradi huu unajengwa gharama ya Euro milioni 13, fedha ambazo zimefadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya kupitia Mpango wa Maendeleo ya Millenium na unatekelezwa kwa kushirikiana na serikali ya Ujerumani kupitia KfW (Benki ya Maendeleo ya Ujerumani).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.