Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe William Lukuvi amezitaka Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kuhakikisha zinaongeza ukusanyaji wa maduhuli kwani kwa sasa yapo chini sana.
Mhe. Lukuvi ambaye amefanya ziara ya siku moja Mkoani Lindi katika Wilaya ya Lindi alisema kuwa bado hali ya makusanyo ya maduhuli na kodi za ardhi yapo chini ukilinganisha na malengo Mkoa uliojiwekea. Ambapo kwa mwaka 2016/2017 Mkoa ulikuwa na lengo la kukusanya 3,270,000,000.
Lakini mpaka tarehe 27 Aprili 2017 Halmashauri za Wilaya na Manispaa zilikuwa zimekusanya shilingi 2,245,090,359 ikiwa ni asilimia 68.66 ya lengo la makusanyo. Hivyo Mhe. Lukuvi amezitaka Halmashauri zote kuhakikisha ifikapo tarehe 30 Juni 2017 zimekamilisha kukusanya kiasi kilichobakia.
Pia ameziagiza Halmashauri kuongeza kasi ya upimaji wa viwanja na mashamba ikienda sambamba na umilikishaji wake kwani kwa kufanya hivyo ndio kutato fursa kwa wananchi wamiliki wa ardhi kuweza kukopesheka kwenye mabenki. Vilevile kuuweka mji katika mpangilio unaoeleweka.
“Kwa kutopima viwanja mnafanya mji kujengwa kiholela hivyo ukatazaji watu kujenga kiholela uende sambamba na kasi ya upimaji maeneo na umilikishaji”, alisema Mhe. Lukuvi. Vilevile aliwaagiza Watendaji wa Kata na Mitaa katika miji kuhakikisha wanatoa taarifa pale wanapoona ujenzi wa kiholela unapotaka au kuanza katika maeneo yao ili hatua zichukuliwe kwa wakati.
Aidha, amempongeza Mhe. Zambi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutatua migogoro ya ardhi katika mkoa na kumuahidi kuwa yeye pamoja na Wizara wataendelea kutoa ushirikiano pale utakapohitajika. Vilevile aliuagiza Mkoa kuyapitia upya mashamba yote yasiyoendelezwa na kujua kama yanalipiwa kodi. Pia kujua kama kuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa na kama bado basi wahusika wapewe ilani na taarifa hiyo apatiwe.
Pia Mhe. Lukuvi amesema tayari wameshatangaza katika gazeti la serikali uanzishaji wa mabaraza ya ardhi katika Wilaya ya Ruangwa na Nachingwea. Lakini amekubali kwenda kulifanyia kazi ombi la Mkuu wa Mkoa la kuanzisha mabaraza ya ardhi katika Wilaya ya Liwale na Kilwa kutokana na umbali uliopo kufika Lindi ambako kwa sasa ndio lipo baraza la ardhi.
Katika taarifa ya Mkoa iliyosomwa kwake na Katibu Tawala Mkoa, Ndg. Ramadhani Kaswa ilibainisha maendeleo ya sekta ya ardhi. Ambapo ilibainisha masuala ya hali ya watumishi, maeneo ya uwekezaji mkubwa, upimaji wa ardhi na viwanja, uandaaji wa hati miliki za viwanja na hatimiliki za kimila, ukusanyaji wa maduhuli na kodi za ardhi na utengaji wa maeneo ya viwanda na maeneo ya wajasiriamali.
Pamoja na taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zambi alimueleza Waziri kuwa Mkoa bado unaendelea kushughulikia migogoro ya ardhi ambapo aliitaja baadhi ya migogoro kama; mgogoro wa mpaka kati ya Lindi na Mtwara, mgogoro wa mpaka kati ya Kilwa na Rufiji, na migogoro ya mpaka kati ya wananchi na JWTZ katika Wilaya za Kilwa, Lindi na Nachingwea. Migogoro yote hii inaendelea kushughulikiwa katika ngazi ya mkoa.
Mhe. Lukuvi alitembelea na kukagua mfumo wa makusanyo ya kodi za ardhi katika masijala za ardhi zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na Manispaa ya Lindi. Ambapo pia aliendelea kusisitiza Halmashauri ziongeze kasi ya upimaji, utoji hati na ukusanyaji wa maduhuli na kodi za ardhi.
Vilevile alitembelea ofisi za Shirika la Nyumba ambapo baada ya kupata taarifa, Mhe. Lukuvi aliwashauri katika majengo yao yaliyochoka waanze kuangalia uwezekano wa kuwapata wadau ambao watashirikiana nao katika kuwekeza kwenye maeneo hayo. Hapa pia alimwagiza mkurugenzi wa manispaa kuhakikisha wanawapa ilani wale wote wenye majengo chakavu katika miji na kuanza kutoa vibali vya ujenzi wa aina ya majengo kulingana na mpango wa matumizi ya ardhi wa eneo husika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.