Mhe. Lukuvi: Wananchi msibadilishe matumizi ya msitu wa Mbumbilaa
Wananchi wa kijiji cha Nanjilinji A na kijiji cha Mirui wameagizwa kutobadilisha matumizi ya ardhi ya msitu wa Mbumbilaa ambao awali ulikuwa unamilikiwa na kijiji kimoja.
Maagizo haya yametolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi wakati alipotembelea vijiji hivyo kwa ajili ya kutao ufafanuzi kuhusu mgogoro wa mpaka wa ardhi uliopo kati ya kijiji cha Nanjilinji A kilichopo wilaya ya Kilwa na kijiji cha Mirui kilichopo wilaya ya Liwale ambapo aliwaeleza wananchi hatua ambazo zitachukuliwa ili kumaliza mgogoro huo.
Msitu huu wenye ukubwa wa hekta 64,000 awali ulikuwa unamilikiwa na kijiji cha Nanjilinji A lakini baada ya wataalam kupitia upya ramani zilizopo, wakabaini kwamba asilimia 30 ya msitu huu ipo katika kijiji cha Mirui. Mhe. Lukuvi aliwaeleza kuwa mpaka utakaowekwa utaonyesha eneo hilo na kwamba kuanzia sasa kijiji cha Mirui kitaanza kunufaika na msitu.
“Kwa kuwa wataalam wamebaini kuwa asilimia 30 ya msitu wa Mbumbilaa upo ndani ya kijiji cha Mirui, kuanzia leo tarehe 10/07/2018 kijiji cha Mirui kitaanza kunufaika na mapato yatokanayo na msitu wa huu kulingana na asilimia ya msitu uliopo katika kijiji cha mirui”, alisema Mhe. Lukuvi.
“Aidha, ni marufuku kwa kijiji cha Mirui na Nanjilinji A kubadilisha matumizi ya msitu wa Mbumbilaa, eneo la msitu ni lazima liendelee kulindwa na pande zote za vijiji kwa kuzingatia mipaka mtakayoonyeshwa na wataalam kwa mujibu wa ramani”, alisisitiza Mhe. Lukuvi.
Katika kutatua mgogoro huu wa mpaka, ilibainika kuwa mpaka wa vijiji hivyo vya mpakani kwa mujibu wa tangazo la serikali la mwaka 2007 ulikuwa umekosewa kwa kutozingatia mipaka ya kiwilaya na hivyo unatakiwa kufanyiwa marekebisho kwa kufuata tangazo la serikali la mwaka 1980 iliyotangaza mpaka kati ya wilaya ya Kilwa na Liwale. Hivyo ramani ya kijiji cha Mirui inatakiwa kurekebishwa kwa kutengenezwa nyingine pamoja na hati wakati ramani ya kijiji cha Nanjilinji A inatakiwa kutengenezwa mpya kwani kijiji hakina ramani wala hati.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewasihi wananchi katika vijiji hivi kuhakikisha wanawapa ushirikiano wataalam wa ardhi ambao watakwenda kuweka alama za mipaka. Aidha, amewataka Wakuu wa Wilaya za Kilwa na Liwale pamoja na wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia kuhakikisha alama za mipaka, upimaji na upatikanaji wa hati linaanza kutekelezwa tarehe 20 Julai 2018.
Pia Mhe. Zambi amemuhakikishia Waziri kuwa mkoa utaendelea kushughulikia malalamiko na kutatua migogoro ya ardhi iliyopo na kuhakikisha utaratibu unawekwa ili kuzuia migogoro mipya isijitokeze.
Wananchi katika vijiji vyote viwili walikubaliana na maelezo ya waziri kuhusu utatuzi wa mgogoro wa mpaka. Aidha, wananchi wa pande zote mbili wamempongeza juhudi kubwa zilizofanywa na wizara, mkoa na wilaya katika kutatua mgogoro huu uliodumu kwa muda mrefu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.