Mhe. Majaliwa: Limeni muhogo soko lipo.
Wananchi wa mkoa wa Lindi na Mtwara wametakiwa kuongeza uzalishaji wa muhogo kwa kuwa tayari soko limeshapatikana.
Hayo yamesemwa na Mhe. Kassim M. Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kuchakata muhogo cha kampuni ya Cassava Starch of Tanzania Corporation Limited (CSTC) kilichopo katika kijiji cha Mbalala, kata ya Nyengedi mkoani Lindi.
Mhe. Majaliwa amesema lengo la serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ni kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kuhamasisha wadau mbalimbali wa maendeleo kuja kuwekeza. Ujenzi huu wa kiwanda utasaidia katika uongozaji wa thamani wa mazao yetu badala ya kuyasafirisha kama maligafi.
“Zao la muhogo kwa mkoa wa Lindi limekuwa likizalishwa kwa wingi na kwa asilimia kubwa limekuwa likitumika kama chakula, sasa wakulima wetu wanatakiwa kulima muhogo kwa wingi kama zao la biashara na soko la uhakika tayari tunalo hapahapa”, alisema Mhe. Majaliwa.
Mhe. Majaliwa pia amekipongeza kituo cha utafiti wa mazao ya kilimo cha Naliendele kilichopo mkoani Mtwara kwa kazi nzuri ya utafiti wa mbegu za mazao mbalimbali wanayoifanya na kusema kuwa kituo hicho ndicho kilichotafiti mbegu bora za muhogo zenye uwezo wa kuzalisha tani 20 hadi 50 kwa hekta.
Naye Balozi wa ufaransa nchini nchini Tanzania, Balozi Frederic Clavier amesema Serikali ya Ufaransa ipo tayari kumuunga mkono Rais Dkt. Magufuli katika mkakati wake wa kukuza uchumi hadi kufikia uchumi wa kati kwa kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.
Balozi Claver kusema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ni ushuhuda tosha wa ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ufaransa kupitia sekta ya kilimo.
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba amewashukuru wawekezaji hao kwa uamuzi wao wa kujenga kiwanda cha kuchakata muhogo nchini kwa kuwa wamewezesha wakulima wa zao hilo kupata soko la uhakika na vijana wengi kupata ajira.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya CSTC, Christophe Gallean alisema kiwanda hicho ambacho kilianza kujengwa mwaka 2012 kinazalisha unga wa muhogo wenye kiwango cha juu cha ubora na kinauza unga huo katika nchi za Afrika Mashariki, Kusini, Mashariki ya Kati, Ulaya na Marekani.
Pia alieleza kuwa kiwanda kiwanda kina wafanyakazi zaidi ya 420 ambapo Watanzania ni asilimia 97. Kiwanda hiki kina uwezo wa kuchakata tani 60 za muhogo mbichi kwa siku, ambao ni sawa na tani 25 za unga bora wa muhogo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.