Mhe. Majaliwa: Fanyeni kazi kwa ushirikiano.
Watendaji wa mkoa wa Lindi wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano katika kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo katika mkoa.
Agizo hilo limetolewa na Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao chake na wakuu wa wilaya, kamati ya ulinzi na usalama, viongozi wa CCM (M), mstahiki meya wa manispaa ya Lindi, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa sehemu na vitengo wa sekretarieti ya mkoa kikao kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Mhe. Majaliwa amesema viongozi wanatakiwa kufanya kazi kuwa ushirikiano na mshikamano ili shughuli za maendeleo ziweze kufanikiwa. Katika mkoa wa lindi miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo zinafanyika hivyo viongozi pamoja na wataalam wao wametakiwa kushirikiana kusimamia na kufuatilia.
“Viongozi msipofanya kazi kwa ushirikiano, shughuli za maendeleo lazima zitakwama kwani mtakuwa mnaishia kulaumiana na sio kusimamia na kufuatilia ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika maeneo yenu”, alisema Mhe. Majaliwa.
“Ushirikiano na mshikamano huu usiishie kwenu viongozi bali unatakiwa kushuka chini kwa watendaji wenu mnaowaongoza, hivyo ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi, viongozi, watendaji na wananchi katika maeneo yenu”, aliongeza Mhe. Majaliwa.
Katika kikao hicho viongozi walielezwa kuhusu kuanza maandalizi ya miradi ya mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2019 ambao utazimwa katika mkoa wa Lindi. Hivyo viongozi wa wilaya wametakiwa kusimamia na kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa katika halmashauri inakuwa ni ya viwango vinavyotakiwa ili utakapofika muda wa kuchagua miradi kusiwe na kazi.
Katika kikao hicho Mhe. Majaliwa alionyesha kuchukizwa na namna baadhi ya halmashauri kufanya vibaya kwenye miradi iliyopitiwa na mwenge wa uhuru kwa mwaka 2018 na hivyo kusababisha mkoa kutoka nafasi ya pili 2017 hadi nafansi ya kumi na mbili mwaka 2018.
Aidha, viongozi wa CCM wametakiwa kuwa makini katika kusimamia miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanyika katika mkoa na pale wanapoona kuna kasoro ya aina yoyote watoe taarifa mapema ili utatuzi uweze kufanyika kwa haraka.
Mhe. Majaliwa katika kikao hicho alitoa taarifa rasmi ya serikali kuhusu maamuzi ya kutofanya maadhimisho ya sherehe za uhuru za tarehe 9 Decemba kwa namna ilivyozoeleka badala yake kila mkoa na wilaya wataadhimisha kwa kupanga shughuli mbalimbali za kufanya na kutoa taarifa ya utekelezaji wake. Aidha, fedha shilingi 995,182,500 zilizokuwa zitumike kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo sasa zitatumika kujenga hospitali mpya ya Uhuru (UHURU HOSPITAL) itakayojengwa mkoani Dodoma njia ya kuelekea Dar es Salaam.
kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey W. Zambi alimueleza Waziri Mkuu kuwa katika ziara mbalimbali za kikazi alizozifanya katika wilaya, huwa anakutana na watendaji wa serikali ambapo suala la ushirikiano amekuwa akilihimiza sana. Aidha, amemuahidi kuwa ataendelea kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika mkoa ikiwa ni pamoja na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.