Mkuu wa wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga amewataka wananchi wa Lindi kujenga utamaduni wa kufanya utalii wa ndani katika maeneo mbalimbali ya kitalii ikiwemo maeneo ya fukwe za bahari na mbuga za wanyamapori zilizopo ndani ya mkoa wa Lindi.
Mhe. Ndemanga ameyasema hayo alipokuwa akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi katika tamasha la utalii linalojulikana kama Kuchele Lindi Utalii Festival lililofanyika katika fukwe za bahari za kijiji cha Shuka kilichopo katika Halmashauri ya Mtama, mkoa wa Lindi.
“Niwatake wanakijiji wa Shuka na wanaLindi kwa kiujumla kujenga utamaduni wa kjufanya utalii wa ndani, kwa kutembelea vivutio mbalimbali za utalii kama utalii wa fukwe za bahari, mbuga za wanyama na maeneo mengine ya kihistoria. Sisi wenyewe tuwe na utamaduni wa kuvitembelea kwanza vivutio vyetu na tuvijue, mkoa wetu umejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kihistoria na ukisoma historia ya nchi hii ni mkoa wa Lindi pekee katika wilaya ya Kilwa ndo ulianza kuijua na kuitumia pesa yake” Mhe. Ndemanga.
“Ukienda kule Liwale unakutana na mbuga ya Selous, ukienda Nachingwea unakutana na historia kubwa ya ukombozi wa Afrika,nchi ya Afrika kusini na nchi nyingi za Afrika zimepata ukombozi kupitia Nachingwea hakuna viongozi waliodai uhuru ambao hawajakaa Nachingwea,kwaiyo tunawaomba wanaLindi tuchangamke kukaribisha wawekezaji ambao watatusaidia pia kukuza utalii katika mkoa wetu,na niwaambie tu serikali ya mkoa imekusudia kushirikiana na watu na sekta binafsi kukuza na kuutangaza utalii ndani ya mkoa wetu” Ameongeza.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewahasa wananchi kutunza mazingira kwa kuacha kukata miti ovyo na kufanya usafi katika maeneo ya fukwe za bahari ili kuzidi kuvutia zaidi watalii katika maeneo yao.
“Lakini ndugu zangu wa Shuka na wanaLindi, utalii huu hauwezi kuwa mzuri kama hatujatunza mazingira yetu, twendeni tutunze mazingira yetu, tutunze uoto wa asili,tufanye usafi kwenye beach zetu ili wawekezaji hawa na watalii wafurahi wakiwa kwenye haya maeneo,tusikate miti hovyo, tusikate mikoko mana ndiyo inayopelekea kuzaliana kwa samaki. Na zaidi tujitahidi kuboresha na kulinda usalama wa watu na mali zao na sisi kama serikali tumejipanga zaidi kuboresha usalama katika mkoa wetu”
Naye, mkurugenzi mkuu wa Kuchele Beach Dkt. Bora Haule (PhD) amesema tamasha la kuchele utalii festival linalenga zaidi kutangaza fursa za utalii zilizopo ndani ya mkoa wa Lindi pamoja na fursa za uwekezaji katika utalii wa bahari hasa fukwe nzuri na safi zilizopo ndani ya mkoa.
“Uchumi wa buluu ni moja ya vipaumbele vya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na tumekuwa na fursa za ufugaji wa majingoo bahari, kaa, ulimaji wa mwani ambazo ni fursa zinazopaswa kuchangamkiwa na wananchi wote. Aidha, uchumi wa buluu una fursa kubwa ya biashara, hivyo ni lazima tuhamasishe wananchi waweze kutumia fursa zinazopatikana humo ili waweze kuzalisha kwa wingi na kukuza vipato vyao” amesema Dkt. Bora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.