Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Hamis Nderiananga amezitaka kamati zinazoshughulikia maafa Mkoani Lindi kuendelea kupanga mikakati madhubuti katika kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa sambamba na kukumbusha wajibu wa taasisi za kisera na taasisi katika kuchukua hatua za kuokoa maisha na mali za wanajamii.
Naibu Waziri ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao kazi cha kujenga uwezo kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa mkoani Lindi kilichoratibiwa na Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo kimelenga kuzifikia kamati za maafa kwa ngazi za mikoa na kuzijengea uwezo wa kukabiliana na maafa pindi yanapotokea ambapo Mhe. Ummy amezikumbusha kamati hizo umuhimu wa kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa kuzingatia madhara yatokanayo na maafa hayo.
"Kikao chetu cha leo kimezingatia wajibu mlionao kwa kuzingatia mujibu wa sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake, ambayo imeanzisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya,Kata na Vijiji huku Jukumu la msingi la kamati hizo nikuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kwa lengo la kukabiliana na kurejesha hali ya awali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea" Alieleza.
Aidha, Naibu Waziri amekumbushia wajibu wa kila mmoja katika eneo lake la kazi kuendelea kuchukua hatua stahiki endapo maafa yatatokea huku akielezea kuwa mfumo wa serikali unatambua na kuzingatia wajibu wa sekta binafsi na taasisi zenye jukumu kisera na kisheria katika kuchukua hatua stahiki ili kuokoa maisha na mali za jamii.
"Uzoefu unaonyesha kuwa kuchukua hatua za mapema ili kuzuia au kupunguza madhara zimekuwa na gharama nafuu kuliko kusubiri na kuchukua hatua pale maafa yanapotokea ambapo serikali imekuwa ikilazimika kutumia pesa nyingi na hapa nipongeze juhudi na hatua hizi za mapema zinazofanywa na serikali chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuimarisha uchumi na huduma za kijamii katika ujenzi wa Taifa letu zinakuwa stahimilivu dhidi ya maafa" Mhe. Ummy Nderiananga.
Aidha, Mhe.Shaibu Ndemanga, Mkuu wa Wilaya ya Lindi akitoa salamu za Mkoa wa Lindi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi ameeleza kuwa Mkoa umeendelea kujipanga na kuchukua hatua zote za tahadhari katika kukabiliana na maafa mbalimbali ikiwemo tahadhari za mvua za Elnino zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kama ilivoelekezwa na Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa, na kuhaidi kuendelea kuzingatia umuhimu wa kuchukua tahadhari za mapema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.