Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amekabidhi rasmi magari 18 yaliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuboresha huduma za afya katika mikoa ya Tanzania ikiwemo Mkoa wa Lindi.
Akikabidhi magari hayo, Mhe.Telack amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na anavyowajali wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa kuwapatia jumla ya magari 18 ya kisasa ambapo magari 10 yatatumika kwa shughuli za ufuatiliaji na magari 8 yatatumika kubebea wagongwa (ambulance) .
Mhe. Telack amesisitiza kuzingatia matumizi mazuri ya magari hayo ambayo yametengenezwa maalum kwa kusafirisha na kutoa huduma kwa mgonjwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Awali, akitoa taarifa ya Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dkt. Kheri Kagya amepongeza juhudi na dhamira nzuri ya serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma hizo.
Dkt. Kagya ameendelea kueleza kuwa vifaa tiba hivyo vinaenda kuhakikisha upatikanaji wa huduma za vipimo na matibabu ambayo awali havikua vinapatikana katika hospitali za wilaya na rufaa ndani ya mkoa ikiwemo Huduma za vipimo vya mionzi ya CT-Scan, Ultrasound, X-ray pamoja na mashine 10 za usafishaji wa damu yaani Dialysis Machine ambazo hutumika hususan kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo.
Vilevile, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi ameishukuru na kupongeza juhudi endelevu za kuboresha huduma za afya ikiwemo na uletwaji wa magari 18 katika mkoa wa Lindi ambayo yanahusisha na magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) ya kisasa yenye uwezo na vifaa vinavyowezesha utoaji huduma za dharula kwa wagonjwa.
Makabidhiano hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya na Mkoa wakiwemo Wabunge, Wakuu wa wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi ambapo wote wametilia mkazo kuhusu usimamizi na matumizi sahihi ya magari hayo katika kuboresha huduma za afya kwa wanajamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.