Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack jana alhamisi ametoa vyakula kwa ajili ya kusheherekea siku kuu ya Eid kwa wanafunzi wa bweni wa Shule ya Lindi Sekondari pamoja na wafungwa waliopo gereza la Lindi.
Akikabidhi vyakula hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amesema kuwa Mhe. Zainab Telack ametoa mchele jumla kilogram 150, nyama kilogram 80 na mafuta Lita 10 kwa ajili ya taasisi zote mbili.
Mhe. Ndemanga ameongeza kuwa vyakula hivi vimetolewa na Mkuu wa Mkoa ili kuwawezesha wanafunzi wa bweni zaidi ya 300 ambao wameshindwa kuungana na familia zao katika Sherehe za Eid. Pia amewakumbuka wafungwa waliopo gereza la Lindi ili wapate fursa ya kusheherekea siku kuu hiyo sambamba na wenzao waliopo mtaani.
Wakipokea vyakula hivyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Lindi Mwalimu. Ramadhan Abdallah Divelle amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuweza kutoa chakula hicho kwa wanafunzi wa Shule hiyo.
Akitoa shukrani zake kwa niaba ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Lindi, Mwanafunzi Noel Henny Lymo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa upendo aliouonesha kwa wanafunzi wa Shule hiyo. Mwanafunzi Lymo ameongeza kuwa Mwenyezi Mungu ambariki Mkuu wa Mkoa kwa kutoa chakula katika siku muhimu kwa jamii ya kiislam sambamba na ndugu zao wakristo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Lindi SP. Fadhili Juma Donile akipokea vyakula hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi La Magereza Mkoa wa Lindi ametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa kwa kutoa msaada wa vyakula kwa wafungwa ambao utawapatia furaha sawasawa na wananchi wengine waliopo majumbani.
Hata hivyo, Baraza la Waislam, BAKWATA limetangaza jana alhamisi kutoandama kwa mwezi hivyo Siku kuu ya Eid haitokuwa Ijumaa na badala yake itakuwa Jumamosi ya tarehe 22 Aprili 2023.
ReplyForward |
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.