Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewaasa watumishi wanaostaafu kuitumikia Serikali katika Mkoa wa Lindi kufanya maamuzi ya kujenga, kuishi na kuwekeza Mkoani hapa.
Mhe. Telack ameyasema hayo jana jumapili tarehe 18 Februari 2024 alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya kuwaaga watumishi waliostaafu mwaka Jana 2023 kuitumikia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ya Lindi iliyoenda sambamba na kuukaribisha mwaka mpya 2024.
Akizungumza mbele ya wastaafu na washiriki katika sherehe hiyo, amesema kuwa mtumishi yeyote anayestaafu kazi katika Mkoa wa Lindi ni vyema akafanya maamuzi sahihi ya kubaki na kuishi Mkoani hapa.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Lindi ni moja ya mikoa michache nchini ambayo bado ina fursa nyingi za kiuchumi ukilinganisha na mikoa mingine ambayo inahitaji nguvu kubwa kupata na kutumia fursa za uwekezaji.
Amewaeleza wastaafu kuwa, Lindi ndio sehemu pekee yenye ardhi ya kutosha na inapatikana Kwa gharama nafuu ukilinganisha na maeneo mengi wanayokimbilia wastaafu wengi kama vile Dar es salaam.
Wastaafu walioagwa rasmi hapo Jana ni pamoja na Ndg. Apolonalius Temu aliyekuwa Muhasibu, Ndg. Edwin Ngongolowo aliyekuwa Muhasibu, Bi. Hawa Khatib aliyekuwa mtunza kumbukumbu, Ndg. Gaudence O. Nyamihura aliyekuwa Afisa Maendeleo Mkuu, Ndg. Khatib Tuki aliyekuwa Afisa Elimu, Ndg. Josh Mwaraha aliyekuwa Afisa Tarafa Maandalizi pamoja na Ndg. Selemani Msafiri aliyekuwa Dereva Mwandamizi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.