Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewataka wakulima wa mwani Mkoa wa Lindi kubadili fikra tegemezi ili waweze kujisimamia kwenye mahitaji ya pembejeo.
Mhe. Telack ameyasema hayo Leo katika kongamano la Uvuvi lililofanyika Wilayani Kilwa baada ya kuibuka hoja ya mgongano Kati ya wanunuzi na wakulima wa zao hilo. Changamoto hiyo inasababishwa na wakulima wa zao hilo kukiuka mkataba unaowataka kumuuzia mazao ya mwani mnunuzi aliyewapatia pembejeo kwa ajili ya uzalishaji wa zao hilo. Hivyo baadhi ya wakulima baada ya kuvuna mwani huwauzia wanunuzi wengine tofauti na mnunuzi aliyeingia mkataba na wakulima hao kwa kuwapatia pembejeo.
Kutokana na changamoto hiyo, Mhe. Telack amewataka wakulima kubadilika na waanze kujiwekea fedha benki kidogo kidogo zitakazo wawezesha kununua pembejeo zao wenyewe. Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo itasaidia kupanda Kwa bei ya zao hilo ambapo Kwa Wilaya ya Kilwa ni Tsh. 1,000/= Kwa kilo moja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mtandao usio wa kiserikali, LANGO Ndg. Michael Mwanga amesema kuwa taasisi hiyo imewasaidia wakulima wa mwani wa Mkoa wa Lindi kwa kuwapatia zana za Kilimo hicho ikiwemo kamba, taitai pamoja na viatu vya cha-cha-cha zenye thamani ya Tsh.32,400,000. Ameongeza kuwa taasisi hiyo pia inaendelea kuwapatia mafunzo ya uongezaji dhamani wa zao hilo kwa kuzalisha bidhaa za mafuta, sabuni, unga wa zao hilo na bidhaa zingine. Ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni uboreshaji wa bei ya zao hilo kwa kuuza bidhaa na kuachana na uuzaji wa mwani ghafi wenye bei ndogo.
Awali akiwasilisha taarifa ya Uvuvi ya Mkoa wa Lindi, Afisa Uvuvi wa Mkoa Ndg. Jumbe Kawambwa amesema kuwa uzailishaji wa mwani umeongezeka kutoka tani 993,064 zenye thamani ya Tsh. 640,782,400 kwa mwaka 2020/21 hadi tani 1,608,770 zenye thamani ya Tsh. 927,066,508 kwa mwaka 2021/22.
Ndg. Kawambwa ameongeza kuwa ongezeko hilo la uzalishaji limetokana na pembejeo za Kilimo cha mwani zilizotolewa kwa wakulima kutoka Wizara ya MIfugo na Uvuvi. Hata hivyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea na mchakato wa kutoa mikopo nafuu ya boti za uvuvi na pembejeo za mwani.
Aidha, Ndg. Kawambwa ametoa wito kwa wakulima wa mwani na wavuvi kujiunga kwenye vikundi na ushirika ili waweze kupata fursa za kuongeza mitaji kutoka taasisi mbalimbali za mikopo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.