Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewataka Wakuu wa Wilaya za Lindi kuhakikisha wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza na darasa la kwanza wanajiunga na masomo kwa 100%.
Mhe. Telack ametoa maelekezo hayo leo asubuhi katika hafla fupi ya kuwaapisha Wakuu wa Wilaya wapya walioteuiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 25 Januari 2023. Wakuu wa Wilaya walioteuliwa kwa Mkoa wa Lindi ni Mhe. Goodluck Asaph Mlinga anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Liwale pamoja na Mhe. Christopher Ngubiagai anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa. Aidha, Mhe. Mohamed Hassan Moyo anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea baada ya kuhamishiwa kutoka Wilaya ya Iringa.
Katika hafla hiyo, Mhe. Zainab Telack amewasisitiza Wakuu wa Wilaya hao kusimamia na kuhakikisha wanafunzi wote wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza na darasa la kwanza wanaanza masomo mara moja. Pia kuhakikisha wanafunzi hao wanahudhuria darasani kwa siku zote 194 za masomo kwa mwaka mzima.
Pamoja na suala hilo la wanafunzi wanaanza masomo, Mhe. Telack amewaelekeza Viongozi hao kusimamia uanzishwaji wa mashamba shuleni kwa ajili ya kuzalisha mazao ya chakula na kuondoa changamoto ya njaa kwa wanafunzi wakati wa mchana.
“ Wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wawe darasani, lakini wale wenye sifa waliofikia umri wa kuanza darasa la kwanza wote wawepo darasani.”
“Tumekubaliana shule zetu zina maeneo makubwa sana, tumekubaliana Wakuu wa Shule waanzishe mashamba ili watoto wapate chakula cha mchana……nendeni mkasimamie.” Amesema Mhe. Telack.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Ngubiagai amesema kuwa suala la elimu ni haki ya msingi ya mtoto hivyo atatumia taratibu zote zilizowekwa ikiwemo sheria kuhakikisha mzazi yeyote mwenye mtoto anaetakiwa kuanza darasa la kwanza, darasa la awali au kidato cha kwanza anamfikisha mwanae shuleni kuanza masomo mara moja.
Akitangaza vita kali dhidi ya wazazi wanaowanyima haki ya elimu watoto, Mkuu wa Wilaya ya Nachngwea Mhe. Mohamed Hassan Moyo amesema kuwa ustawi wa mtoto na haki ya mtoto lazima visimamiwe ipasavyo hivyo litafanyika zoezi la kuwatambua na kuwafikisha shuleni watoto wote wanaotakiwa kuanza masomo.
“Suala la elimu ni mapambano, ustawi wa mtoto na haki ya mtoto lazima visimamiwe, kwa hiyo mzazi yeyote yule atakae sababisha mwanae kutokwenda shule kwa sababu zozote zile hatutoweza kumfumia macho………….suala la mwanafunzi kwenda shule ni suala msingi na tutafuatilia nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.